LA PAZ, BOLVIA
RAIS wa zamani wa Bolivia, Evo Morales amesema yuko tayari kurejea nchini mwake haraka iwezekanavyo, wakati wafuasi wake wakikabiliana na polisi dhidi ya kiongozi aliyejitangaza mwenyewe Jeanine Anez.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mexico City, Morales ametaka kufanyike mazungumzo baina ya pande zote, na kusema atarejea nchini endapo ataombwa na watu wake.
Watu wawili walipoteza maisha katika ghasia baina ya wafuasi wa rais huyo na serikali ya muda, sambamba na vikosi vya usalama.
Idadi jumla ya watu waliouawa sasa imefikia 10 wakati wa wiki tatu za maandamano.
Mabomu ya kutoa machozi yalifyatuliwa hapo juzi mjini La Paz, wakati wa maandamano ya kutaka rais huyo wa zamani kurejeshwa madarakani.
Morales alikuwa rais wa Bolivia kwa miaka 13 na alikimbilia uhamishoni siku ya Jumanne na kuchochea makamu wa rais wa Seneti Anez kujitangaza rais.