32.3 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Mongella: Uokoaji haujawahi kusitishwa

Na AGATHA CHARLES


MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amesema shughuli ya uokoaji na kutoa miili iliyozama majini kutokana na ajali ya Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Ziwa Victoria haijawahi kusitishwa bali inaongozwa kitaalamu.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana akiwa eneo la tukio baada ya kudai kuwapo upotoshaji kuhusu jambo hilo.

“Mimi niseme kwamba tusipotoshe, uokoaji haujawahi kusitishwa, kinachofanyika ni kwamba ni shughuli ya kitaalamu, shughuli hii ya uokoaji haifanywi na mkuu wa mkoa au sijui kiongozi mwingine.

“Shughuli hii inafanywa na wataalamu, hawa wazamiaji wote ni wataalamu kwa hiyo ikifika mahali wakasema sasa kuingia chini ya chombo haiwezekani kitaalamu, huwezi kutoka mkuu wa mkoa ukasema ingia,” alisema.

Mongella aliwashukuru wananchi na Watanzania pamoja na wanahabari kwa kushiriki kimamilifu tangu mwanzo wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine, mkazi mmoja wa Mwanza aliyepiga simu chumba cha habari (hakutaka jina lake liandikwe gazetini), aliiomba Serikali kuchunguza kama ni kweli kivuko hicho kilifungwa injini mpya.

“Serikali ikianza uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo pia ichunguze kama kweli injini zilizofungwa ni mpya.

“Kwa kawaida kila injini ina serial namba yake ambayo ni tofauti na nyingine, kwa hiyo Serikali ichunguze kama kweli hizo injini zilifungwa katika kivuko hicho kwa sababu kule kuna maboti ya watu binafsi na pengine unaweza kukuta zilichepushwa na kwenda kufungwa katika maboti hayo,” alisema.

Wakati mkazi huyo akisema hivyo, Julai 16, mwaka huu kivuko hicho kilifungwa injini mpya tangu kiliponunuliwa na kuanza kutoa huduma mwaka 2004.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Dk. Mussa Mgwatu, injini hizo zenye thamani ya Sh milioni 191 zilifungwa ili kuongeza ufanisi wake katika kutoa huduma kwa wananchi wa Bugorola na Ukara.

Alisema kivuko hicho kilifungwa injini mbili mpya na giaboksi za aina ya Perkins zenye nguvu ya kilowati 161 kila moja na zilifungwa na mafundi wa Temesa kwa kushirikiana na Kampuni ya Delta Industrial Equipment Limited na kupakwa rangi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles