26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MOKIWA AKUBALI YAISHE

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


ALIYEKUWA Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, amewasilisha barua mahakamani akiomba kuondoa kesi aliyoifungua akipinga kustaafishwa kwa nguvu ili wakamalizane katika nyumba ya maaskofu.

Mokiwa anataka kuondoa kesi hiyo ya madai namba 20 ya mwaka huu aliyofungua dhidi ya Askofu Mkuu wa Makanisa ya Anglikana Tanzania, Mhashamu Dk. Jacobe Chimeledya na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo.

Askofu Mokiwa alifungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akiieleza mahakama, Wakili wa wadaiwa, Gabrieli Masinga alidai  alipokea barua kutoka kwa Wakili wa Askofu Mokiwa, Wakili M.B. Kabunga ikiwaelekeza kuwa kesi iliitwa jana kwa sababu waliwasilisha barua ya kuomba kuiondoa mahakamani.

Alidai barua hiyo ilieleza sababu za kuondoa kesi hiyo ni kutokana na juhudi za kutatua mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.

“Wanaomba kuondoa kesi  wapate muda wa kujadiliana kwa sababu  juhudi haziwezi kufanyika bila kesi hiyo kuondolewa mahakamani,”alidai.

Hakimu Simba alisema barua hiyo hajaiona na kesi hiyo ilipangwa Februari 28 hivyo kuwapo kwao jana mahakama hakutambui.

“Leo mliitwa na nani, mimi siandiki kitu, niandike ili iweje, siwahitaji, kesi imepangwa tarehe 28, pisheni wengine waendelee.  Naona kuna barua ya kumalizana katika nyumba ya maaskofu, kama ni hivyo nawaombea usuluhishi mwema,”alisema Hakimu Simba.

Askofu Mokiwa na wakili wake wote hawakufika mahakamani. Hata hivyo Wakili Masinga alidai askofu huyo anataka kurejeshewa  uaskofu wake, anaomba mahakama itengue uamuzi wa kumstaafisha kwa nguvu.

“Mokiwa alivuliwa uaskofu wake na Januari 7 mwaka huu akakimbilia mahakamani, mambo yanayohusu imani yanatakiwa kushughulikiwa katika nyumba za imani.

“Huwezi kuvuliwa madaraka msikitini ama kanisani ukakimbilia mahakamani, masuala hayo yanajadiliwa katika vyombo husika labda pakiwapo  ukiukwaji wa sheria za nchi,”alidai.
Kwa mujibu wa barua kwa mapadri na maaskofu wote wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, kiongozi huyo alilazimishwa kuvuliwa uaskofu   Januari 7 mwaka huu.

Sababu za kuvuliwa madaraka kwa kiongozi huyo wa muda mrefu wa kanisa hilo ni kudaiwa kuhusika   na ufujaji wa mali za kanisa na matumizi mabaya ya madaraka.

Inadaiwa katika hati kwamba hatua hiyo inatokana na mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake na wadhamini wa makanisa mbalimbali ya Jimbo la Dar es Salaam, ambayo ni Yombo Buza na Magomeni ambao walilalamikia   matumizi mabaya ya madaraka kwa kile walichoita ufisadi huku wakimtaka aandike barua mwenyewe ya kujiuzulu lakini aligoma kufanya hivyo.

Mokiwa anakabiliwa na mashtaka 10 huku shtaka la tatu la uwekezaji, ndilo lililomtia hatiani na yeye kukiri kosa mbele ya tume hiyo ya uchunguzi.

Kesi hiyo itaendelea Februari 28 mwaka huu na  mahakama itaelezwa kama kuna makubaliano ya kuondoa kesi  wakamalizane nje ya mahakama au la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles