Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewaomba Watanzania kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi wanaohitaji huduma hiyo. Wito huo umetolewa Januari 8, 2025, na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Cresencia Mwibari, alipokuwa akijibu hoja za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa eneo la kusubiri huduma katika taasisi hiyo.
Mwibari alisema uhitaji wa damu ni mkubwa, ambapo kwa siku taasisi hiyo hutumia chupa 20 hadi 30 za damu kwa majeruhi wa ajali mbalimbali, hususan za barabarani.
“Napenda kuwahimiza Watanzania kujitokeza kuchangia damu hapa MOI. Tuna wahudumia majeruhi wa ajali waliojeruhiwa vibaya na mara nyingi huwahitaji kuongezewa damu,” alisema Mwibari.
Aidha, aliwakumbusha wachangiaji wa damu wa muda mrefu kuwasilisha kadi zao za uchangiaji katika maabara ya MOI kwa ajili ya uhakiki na uthibitisho wa huduma.
Philimon Ndaki, mmoja wa wagonjwa waliopata huduma MOI, aliwapongeza watumishi wa taasisi hiyo kwa huduma bora, akibainisha kuwa upasuaji wake uliofanyika miaka minne iliyopita ulikuwa wa mafanikio makubwa, na sasa anaendelea kuhudhuria kliniki kila baada ya miezi sita.
MOI imeendelea kusisitiza umuhimu wa uchangiaji damu ili kuboresha huduma kwa majeruhi na wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka.