23.9 C
Dar es Salaam
Thursday, September 29, 2022

MOI SASA KUFANYIA UPASUAJI WA DHARURA WAGONJWA 1,000

NA WAANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


IDARA ya Magonjwa ya Dharura na Ajali (Emergency Medicine) ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu, Mgongo, Ubongo na Uti wa Mgongo Muhimbili (Moi), imehamishiwa katika jengo jingine litakalotoa nafasi kwa wagonjwa wanaopatiwa upasuaji wa dharura kuongezeka kutoka 500 wa sasa hadi 1,000.

Uongozi wa Moi umefanya maboresho kwa kuhamisha idara hiyo kutoka katika jengo lake la zamani kwenda katika jengo jipya la mradi wa Moi Phase III.

Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake, Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi, alisema hatua hiyo imelenga kupanua wigo wa utoaji huduma kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na upasuaji.

“Idara hii ilikuwa katika jengo letu la zamani tangu mwaka 1996, tulikuwa na chumba kimoja pekee cha kufanya upasuaji wa dharura kwa wagonjwa kati ya 23 hadi 40,” alisema.

Mvungi alisema kwa kuhamisha idara hiyo katika jengo jipya, idadi ya vyumba vya upasuaji inaongezeka kuwa viwili tofauti na awali.

“Kwa mantiki hiyo, madaktari wetu watakuwa na uwezo wa kuwafanyia upasuaji wagonjwa wawili kwa wakati mmoja tofauti na zamani ilikuwa akifanyiwa mmoja pekee.

“Kutokana na hali ile, kulikuwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma ya upasuaji wa dharura,” alisema.

Alisema kwa mwezi katika jengo la zamani walikuwa na uwezo wa kuwafanyia upasuaji wa dharura wagonjwa 500 hadi 700.

“Kwa kuhamia katika jengo jipya, tunatarajia idadi ya wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji itaongezeka kufikia 1,000,” alisema.

Mvungi alisema hatua hiyo pia inafanya ongezeko la idadi ya vyumba vya upasuaji kufikia tisa ikilinganishwa na vinane ambavyo vilikuwapo awali.

Alisema hatua hiyo inafanya idadi ya vyumba vya upasuaji Moi kuongezeka kutoka vinane vilivyokuwapo kufikia tisa.

“Zamani tulikuwa na vyumba sita vya upasuaji, sasa tumeongeza vyumba viwili, vimekuwa vinane, na kuna chumba kingine kimoja ambacho tupo katika hatua za mwishoni za matengenezo.

“Chumba hicho kimoja tumekijenga kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, tunazidi kuimarisha huduma zetu,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na ERICK MUGISHA (DSJ), FRANK PETER KAGUMISA (SAUT) na VERONICA ROMWALD

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,298FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles