Moi kuanza upasuaji wa ubongo bila kufungua kichwa Februari

0
739

Aveline Kitomary -Dar es salaam

TAASISI ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (Moi), mwanzoni mwa Februari inatarajia kutoa matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo bila kufungua kichwa baada ya mashine zitakazotumika katika maabara kuwasili nchini.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa kampeni ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’, Mkuu wa Kitengo cha Radiolojia, Dk. Mechric Mango, alisema huduma hiyo itapunguza rufaa za nje ya nchi.

“Hii ni maabara ya kisasa kabisa itakayotuwezesha kufanyika matibabu ya ubongo kwa kupitia mishipa ya damu, itakuwa maabara ya kipekee zaidi hapa nchini na Afrika iko Kenya na Afrika Kusini.

“Maabara hiyo itakuwa na faida ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi, awali wagonjwa waliokuwa wanahitaji upimaji wa mishipa ya damu ya kichwani wote walikuwa wanapelekwa nje ya nchi, kwa hiyo mashine itakapofungwa hawataenda tena nje na itaokoa fedha nyingi,” alisema Dk. Mango.

Dk. Mango alisema uhitaji wa mashine hizo ni mkubwa kutokana na kutoa vipimo na matibabu kwa wakati mmoja.

“Uhitaji wa huduma hiyo ni mkubwa sana, hapa tunashughulika na kichwa, uti wa mgongo na mifupa, sasa wale ambao wana matatizo kwenye ubongo moja wapo ya vipimo vinavyohitajika vikubwa ni hivi.

“Wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu kufanya kazi au mishipa ya damu ambayo sio ya kawaida, hao wanahitaji hiki kipimo.

“Pia mashine hii inatumika kutoa matibabu, kuna wale wenye uvimbe kwenye ubongo, pia tutatumia hii mashine kwa wale wenye mishipa ya damu kwenye uvimbe ili kuzuia damu nyingi isimwagike,” alieleza Dk. Mango.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk. Respicious Boniface alisema mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka minne ni uboreshwaji wa miundombinu, vifaa na karakana ya viungo bandia.

“Serikali ilitoa Sh bilioni 16.5 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa jengo jipya la Moi na kununua vifaa tiba vya kisasa, idadi ya vitanda imeongezeka kutoka 150 hadi 340, pia vitanda vya ICU vimeongezeka kutoka 8 hadi 18 na kuongeza chumba cha maabara kikubwa cha vipimo vya radiolojia, yako mengi, hayo ni machache tu.

“Tumenunua mashine za kisasa kabisa za radiolojia zikiwemo MRI, CT-Scan, Digital X-ray, Portable X-Ray, Ultrasound na C-arm. Mashine sita za dawa za usingizi zimenunuliwa, mashine mbili mpya za kisasa za vipimo vya maabara na vipimo vipya vya kisasa vya mazoezi tiba (physiotherapy),” alibainisha Dk. Boniface.

Alisema katika kipindi cha miaka minne, jumla ya wagonjwa 43,200 wamefanyiwa upasuaji mbalimbali wa kibingwa.

“Waliofanyiwa huduma ya kubadilisha nyonga ni 900, kubadilisha magoti ni 870, upasuaji mfupa wa kiuno ni 618, upasuaji wa ubongo ni 880 na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ni 2,070. Bado idadi ya wagonjwa wa upasuaji imeongezeka kutoka 400-500 kwa mwezi hadi 700-900 kwa mwezi,” alisema Dk. Boniface.

Alieleza kuwa huduma mpya za kibingwa zilizoanzishwa ni upasuaji magoti/mabega kwa njia ya matundu, kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo, kunyoosha vibiongo na upasuaji wa uti wa mgongo kupitia tundu dogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here