Na Mwandishi Wetu
MOHAMMED Morsi ni Rais wa kwanza wa Misri, aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasiakwa kupata asilimia 51 ya kura zote, akimpiku Ahmed Shafik, aliyekuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa Hosni Mubarak.
Morsi alidumu madarakani kwa muda wa mwaka mmoja ambapo aliingia Juni, 2012 na baadaye kuondolewa na jeshi la nchi hiyo Julai 3, mwaka 2013.
CHANZO KUONDOLEWA MADARAKANI
Akiwa madarakani, Morsi alikabiliwa na kashfa mbambali, kubwa zaidi ikiwa ni kuhusishwa kushirikana na vikundi vya kigaidi na ufisadi na hivyo kusababisha kuyumba kwa uchumi wa Misri.
Hali hiyo ilisababisha mamilioni ya wananchi kuingia mitaani kuandamana kwa siku kadhaa kupinga utawala wake na wiki chache baadaye jeshi lilitangaza kumng’oa madarakani na kuipa nafasi serikali ya mpito.
Kiongozi huyo pia alituhumiwa kupuuza amri ya mwisho ya jeshi hilo lililomtaka asulihishe mzozo wa kisiasa nchini humo tangu Hosni Mubarak alipong’olewa madarakani mwaka 2011.
Majeshi yalitoa onyo kwa Morsi kwamba yataingilia kati mzozo unaokumba utawala wake iwapo atashindwa kufikia masharti ya raia katika kipindi cha saa 48.
Ilipofika jioni ya Julai 3, majeshi yaliifuta Katiba na kutangaza kuundwa kwa serikali ya mpito, kabla ya kufanyika upya uchaguzi wa rais.
Morsi alipinga hatua hiyo na kusema kuwa ni sawa na ‘mapinduzi.’
Kiongozi huyo alikamatwa kufuatia amri iliyotolewa na mkuu wa majeshi – ambaye ni rais wa sasa, Abdul Fattah al-Sisi, na kupelekwa sehemu isiyojulikana bila ya mtu yeyote kujua hali yake.
Wafuasi wake waliandamana katika barabara za mji wa Cairo, kushinikiza kuachiliwa kwake na kurudishwa madarakani mara moja.
Jeshi lilitumia nguvu kuvunja mandamano hayo Agosti, 14, na kuwakamata viongozi wa wakuu wa vugu vugu la Muslim Brotherhood.
Watu takribani 1,000 waliuawa katika oparesheni hiyo, ambayo utawala wa mpito ulidai kuwa ni juhudi za kukabiliana na ‘ugaidi.’
ASHTAKIWA KUCHOCHEA MAUAJI
Baada ya kuzuiliwa kwa takribani miezi miwili katika sehemu isiyojulikana, waendesha mashtaka wa serikali walitangaza kwamba Septemba, mwaka 2013, Morsi atashtakiwa kwa kosa la kuwachochea wafuasi wake kumuua mwanahabari na wafuasi wawili wa upinzani na kuamrisha wengine kuteswa na kuzuiliwa kinyume cha sheria.
Mashataka dhidi yake yalihusisha makabiliano kati ya waandamanaji wa upinzani na wafuasi wa kundi la Muslim Brotherhood nje ya makazi ya Rais ya Ittihadiya mjini Cairo, Desemba mwaka 2012.
Kiongozi huyo alishitakiwa pamoja na viongozi wengine 14 wa ngazi ya juu wa Muslim Brotherhood Novemba, mwaka 2013.
APIGA YOWE KIZIMBANI
Wakati kesi yake inasikilizwa kwa mara ya kwanza, Morsi alipiga mayowe kutoka kizimbani akisema yeye ni mhanga wa ‘mapinduzi ya kijeshi’ huku akikataa mamlaka ya mahakama kumfungulia mashtaka.
“Mimi ni Rais wa Jamhuri kwa mujibu wa Katiba ya nchi na nimezuiliwa kwa nguvu,” alisema.
WAHUKUMIWA MIAKA 20 JELA
Aprili, mwaka 2015, Morsi na wenzake walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kuondolewa mashtaka ya uchochezi na kupatikana na makosa ya kuamrisha kuzuiliwa na kuteswa kwa waandamanaji.
Pia alifunguliwa mashtaka mengine ikiwamo kushirikiana na wanamgambo wa kigeni kuwaachia huru wafungwa wakati wa maandamano ya mwaka 2011, kufichua siri za serikali, ubadhirifu pamoja na kutusi mahakama.
GHASIA ZAONGEZEKA
Miaka iliyofuata baada ya Morsi kuondolewa madarakani, Misri ilishuhudia ongezeko la ghasia na mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa Kiislam.
Msako mkali dhidi ya vugu vugu la Muslim Brotherhood ulifanyika huku kundi hilo likitangazwa rasmi kuwa la kigaidi.
Morsi alitoweka machoni mwa umma na kuishia kuonekana kotini alipofunguliwa mashtaka.
Baadaye mtangulizi wake, Hosni Mubarak, aliachiliwa huru kutoka jela baada ya kuonekana kuwa nchi hiyo haikuwa imeendelea mbele kisiasa, licha ya uchaguzi uliomweka Morsi madarakani kwa muda.
HISTORIA YAKE KISIASA
Morsi alizaliwa mwaka 1951 katika Kijiji cha El-Adwah kilichopo Mkoa wa Nile Delta, eneo la Sharqiya.
Alisomea Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Cairo miaka ya 1970 kabla ya kuhamia nchini Marekani ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uhandisi.
Aliporejea Misri, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Zagazig.
Alishikilia nyadhifa kadhaa katika kundi la Muslim Brotherhood, hatimaye kujiunga na kitengo chake cha kisiasa ambapo aliwania kiti cha ubunge akiwa mgombea binafsi. Alishika wadhifa huo kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.
Morsi alipoteza kiti chake cha ubunge nyumbani katika awamu ya pili ya uchaguzi aliyodai ilikuwa na udanganyifu.
Akiwa mbunge, alisifiwa kwa uweledi wake wa lugha na kazi. Aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia Muslim Brotherhood, Aprili 2012 baada ya naibu kiongozi wake, mfanyibiashara Khairat al-Shater, alipolazimishwa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Japo Morsi hakuonekana kuwa na hulka ya kuwa msemaji mzuri, alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Freedom and Justice Party (FJP).
Katika kampeni yake ya uchaguzi, alijinadi kwamba atakuwa mtu atakayeleta mwamko mpya akilinganishwa na viongozi wa zamani kama Hosni Mubarak.
KIFO CHAKE
Morsi alifariki dunia juzi baada ya kuanguka ghafla akiwa mahakamani.
Morsi alifika Cairo Jumatatu ya wiki hii kwa ajili ya kuhudhuria kesi inayomkabili, akidaiwa kushirikiana na kikundi cha kigaidi cha nchini Palestina kinachofahamika kwa jina la Hamas.
Akiwa mahakamani na wenzake, alitakiwa kuzungumza kupitia chumba kilichokuwa na dirisha la wavu, ingawa sauti ilikuwa ikipenya kuwafikia waliokuwa wakiifuatilia kesi hiyo.
Wakati wa mapumziko, alianguka na kuzimia. “Alikimbizwa hospitali, ambako ilithibitika kuwa ameshafariki,” anasema mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali ya Misri.
Akizungumza na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), mwanasheria wake alisema Morsi alizikwa jana asubuhi Mashariki mwa Jiji la Cairo.
Morsi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, ambapo alihitimisha safari yake ya mwisho hapa duniani huku akiwa ameshikiliwa na mamlaka za Misri tangu alipong’olewa madarakani mwaka 2013.
Taarifa ya maofisa wa Serikali ya Misri chini ya Rais Abdel Fattah el-Sisi, zinasema chanzo cha kifo cha kiongozi huyo ni mshtuko wa moyo.
TUHUMA ZA KUUAWA
Kifo cha mwanasiasa huyo kimezifanya mamlaka za Misri zinyooshewe kidole na vikundi vya utetezi wa haki za binadamu, ambao wamepaza sauti kutaka uchunguzi wa kina ufanyike.
Licha ya Serikali ya Misri kusema taarifa hizo kuwa ni za uzushi, vikundi hivyo vinaamini kifo cha Morsi kilisababishwa na mateso aliyopitia kwa kipindi chote cha miaka sita akiwa chini ya ulinzi mkali.
Mbaya zaidi, mtoto wake wa kiume, Abdullah Mohamed Morsi, juzi aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa mamlaka za Misri zimekataa ombi la familia ya kiongozi huyo, kutaka mazishi yake yawe ni ya kitaifa ili kila mwananchi ahudhurie.
Shutuma dhidi ya mamlaka ni kwamba, kwa kipindi kirefu ziliweka sharti la kutokutana na wanasheria wala familia yake, iliyokuwa ikiomba apatiwe matibabu baada ya afya yake kudhoofu.
UKIUKWAJI HAKI ZA BINADAMU
Tangu Morsi na wenzake washikiliwe na vyombo vya dola kwa tuhuma mbalimbali, vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vimekuwa vikiripotiwa mara kadhaa.
Hata alipohukumiwa kifo mwaka 2015, wengi waliikosoa hatua hiyo, wakisema inaakisi kuuawa kwa demokrasia nchini Misri.
“Leo hii, demokrasia imekufa na Mohammed Morsi, mtu aliyekuwa na imani ya kuipagania nchi yake. Kwa sasa, watu wa demokrasia wamekaa kimya juu ya utemi wa jeshi, kuonewa kwa Morsi, watu kutupwa gerezani na hata kuuawa,” anasema Tallha Abdulrazaq, mwandishi aliyejikita katika masuala ya usalama mataifa ya Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake Sarah Leah Whitson, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch kwa Ukanda wa Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii:
“Ni mbaya sana lakini ilitarajiwa kuwa hivyo. Kifo cha Rais wa zamani, Morsi, kinakuja baada ya mateso kutoka kwa serikali, kuwekwa peke yake kwa muda mrefu.
“Uangalizi mdogo wa afya yake, familia kuzuiwa kumtembelea, huku ikiwekewa ugumu kupata msaada wa kisheria, haya yote yamechangia kifo chake.”
Tangu awe mikononi mwa mamlaka ya nchi hiyo kwa kipindi chote cha miaka sita, amekutana na familia yake mara tatu tu.
Katika hilo, Shirika hilo limeuomba Umoja wa Mataifa (UN) kuanza mara moja uchunguzi, likisema kuwa kifo cha Morsi ni mwendelezo wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Misri na magereza kuwa na huduma za afya zisizoridhisha.
LAWAMA KWA MAMLAKA
Shirika la Amnesty International nalo limejitokeza kulaani kifo cha Morsi, likisema suala la uchunguzi halitakiwi kuchukua muda mrefu.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amejitokeza na madai ya aina hiyo, akizitupia lawama mamlaka za Misri, akisisitiza wanapaswa kubebeshwa mzigo wa lawama kwa kifo cha swahiba wake huyo.
Ni kama ilivyokuwa kwa kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Mbunge wa Uingereza, Crispin Blunt, ambaye alikuwa sehemu ya jopo la wanasiasa walioonya mwaka jana kuwa kitendo cha Morsi kuwekwa mafichoni kinahitaji uchunguzi wa kimataifa.