London, England
MWANARIADHA wa Uingereza, Mo Farah, juzi jioni alishinda medali ya sita ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia yanayoendelea England.
Farah (34), alianza vizuri mashindano hayo yaliyoanza juzi, licha ya kukabiliwa na tuhuma za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, hali iliyochangia kutoonekana katika vyombo vya habari.
Lakini Farah aliweka yote hayo pembeni na kuonesha kiwango safi kilichochangia ushindi wake mnono.
Ushindi huo umekuja baada ya miaka mitano kupita kwa nyota huyo kushinda mwaka 2012, wakati Uingereza ilipokuwa mwandaaji wa mashindano ya Olimpiki.
Akizungumza na mtandao wa BBC, Farah alisema: “Ulikuwa usiku mzuri kwangu, kwa kufanya jambo bora zaidi, haikuwa rahisi kushinda kutokana na ubora wa wapinzani wangu. Ni ushindi maalumu kwangu, pamoja na familia yangu.”
Farah pia alishinda katika michuano ya mwaka 2011, 2013 na 2015, na kukamilisha ndoto yake ya kuwa mtu muhimu kwa taifa lake pamoja na wanariadha wachanga.