Mnyukano wa Sugu, Dk Tulia,Sugu

0
778

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), maarufu kwa jina la Sugu, amegoma kusoma hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyohusu bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Tukio hilo lilitokea bungeni jijini jana, baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kumtaka mbunge huyo asome hotuba yake kwa kuruka baadhi ya maeneo ambayo alisema yanakiuka kanuni za Bunge.

Kabla ya tukio hilo, Sugu alikwenda katika meza iliyoko mbele ya Bunge kuanza kusoma hotuba ya kambi yake aliyokuwa ameiandaa.

Baada ya kuanza kuisoma, Naibu Spika alimtahadharisha, kwamba atatakiwa kuruka baadhi ya maeneo kama alivyoelekezwa awali.

“Mhesshimiwa Mbilinyi, tafadhali nakuomba usome hotuba yako kwa kuzingatia maelekezo uliyopewa awali na si vinginevyo,” alisema Naibu Spika.

Baada ya Naibu Spika kutoa maelekezo hayo, Sugu alisema hawezi kusoma hotuba nyingine zaidi ya iliyomo kwenye kitabu chake kwa sababu hiyo mpya anayotakiwa kuisoma hana kitabu chake.

Aliposema hivyo, Naibu Spika alimwagiza Katibu wa Bunge ampelekee mbunge huyo kitabu kipya cha hotuba ya upinzani ambacho ndicho wabunge wote walikuwa wamegawiwa.

Baada ya sekunde chache, mhudumu mmoja wa Bunge alimplekea mbunge huyo kitabu kipya cha hotuba, lakini alipokipokea na kukipekua, alisema hawezi kukisoma kwa sababu sicho alichokiandaa.

“Mheshimiwa Naibu Spika, haya siyo maoni yangu niliyoandaa, sijui mnaogopa nini kwa sababu hapa ni kama tuna mjadala, mimi nasema hivi na nyie mnasema vile.

“Pia nimegundua kumbe ndiyo maana huwa mnachukua mapema hotuba yangu ili muweze kuihariri, hii siyo sawa,” alilalamika Sugu.

Wakati Sugu alipokuwa akiendelea kulalamikia utaratibu huo, Naibu Spika alimkatisha na kumtaka asome hotuba hiyo mpya kwa sababu ndiyo inayotakiwa kusomwa.

“Mheshimiwa Mbilinyi, mwanzoni ulisema hiyo hotuba mpya huna, lakini umeshaletewa. Kwa hiyo soma hiyo uliyoletewa na kama hutaki sema hutaki maana hii haitakuwa mara ya kwanza kutosoma, tafadhali endelea,” alielekeza Naibu Spika.

Pamoja na maelekezo hayo, Sugu alishikilia msimamo wake wa kutosoma hotuba iliyohaririwa na badala yake akaamua kuondoka na kuelekea kwenye kiti chake huku akipigiwa makofi na baadhi ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika aliruhusu mjadala wa bajeti hiyo uanze huku akisema hotuba ya upinzani ambayo haikusomwa, isiingizwe katika kumbukumbu za Bunge kwa kuwa Sugu hakusema kama atataka iingizwe kwenye kumbukumbu hizo.

Hata hivyo, wakati mbunge huyo akichangia bajeti ya wizara hiyo, alisema kitendo cha hotuba ya upinzani kuhaririwa ni kielelezo cha kukandamizwa kwa uhuru wa kujieleza.

Pamoja na hayo, alisema ingawa Serikali inasema Tanzania ina idadi kubwa ya magazeti na vituo vya redio, idadi hiyo haina maana kwa kuwa vyombo hivyo vya habari havina uhuru wa kujieleza kutokana na sheria zilizopo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha  Minja (Chadema), alisema vyombo vya habari nchini havina uhuru wa kuwaeleza wananchi mambo yanayotakiwa kutokana na uwepo wa sheria kandamizi.

Naye Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), alihofia uimara wa timu ya soka ya taifa – Taifa Stars kwa kuwa klabu nyingi nchini zina wachezaji wengi wa kigeni.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa Serikali kuweka masharti ili kumsajili mchezaji wa kigeni nchini, awe anachezea timu ya taifa lake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here