LUSAKA, ZAMBIA
MATOKEO ya awali ya uchaguzi wa urais nchini Zambia yanaonesha kuwa mgombea wa chama tawala cha Patriotic Front (PF), Rais Edgar Lungu amekabana koo na mpinzani wake kutoka chama cha United Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema, akiongoza kwa kura chache.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zambia (ECZ) jana mchana kutoka jumla ya majimbo 69 kati ya 156 ya uchaguzi, Lungu alikuwa akiongoza kwa kura 699,960 dhidi ya kura 644,132 za Hichilema likiwa ni pengo la kura 55,828 tu.
Wagombea wengine saba katika kinyang’anyiro hicho cha urais wameachwa nyuma huku asilimia 56 ya kura ikiwa imebaki kuhesabiwa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UPND, Stephen Katuka ametoa taarifa akisema kiongozi wao ameshinda uchaguzi huo, lakini chama tawala kimechakachua matokeo baada ya kuyachelewesha kwa makusudi.
Katuka alisema kuwa kufikia juzi mchana matokeo yalionesha kuwa Hichilema amepata kura 1,850,000 dhidi ya kura 1,500,000 za Rais Lungu yakiwa ni matokeo yanayotokana na kuhesabiwa kwa asilimia 80 ya kura.
Hichilema mwenyewe jana asubuhi alivamia kituo cha kujumuisha matokeo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mulungushi mjini hapa akiwa na wafuasi wa chama chake, akiilalamikia ECZ kumhujumu.
ECZ imepinga madai ya Hichilema kwamba inakula njama na chama cha Lungu ili kukipatia ushindi licha ya kushindwa, ikiyataja madai hayo kuwa ya kusikitisha.
Wakati Hichilema akivamia kituo hicho, mpinzani wake Lungu alikuwa akihudhuria ibada katika Kanisa la Pentekoste la Ufufuo Eastgate mjini Baulenip.