31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mnyukano kuhojiwa CAG


WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SAKATA la Spika wa Bunge Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge kwa hiari yake ili akahojiwe vinginevyo atafikishwa mbele ya kamati hiyo kwa pingu limezidi kuchukua sura mpya.

Hatua hiyo sasa imemwibua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Ludovik Utoh ambaye amemshauri Spika Ndugai kutumia busara katika kushughulikia suala hilo.

Ndugai alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma akimtaka Profesa Assad kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, kutokana na kauli yake aliyodai kuwa inadhalilisha Bunge.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam jana, Utoh alisema kuwa hawezi kuzungumza kwa sababu CAG analindwa na Katiba.

“‘I can not speak much’ kwa sababu CAG analindwa sana na katiba ibara ya 143 ibara ndogo ya sita, inamlinda sana katiba, lakini kama ulimsikiliza jana Spika naye alisema kanuni za Bunge nazo zinaruhusu yeye kuita mtu yeyote. Hapo itakuwa ni ‘issue’ ya wanasheria, huenda kanuni zinaweza ‘zika-over rule’ katiba,” alisema Utoh.

Alipoulizwa endapo angekuwa yeye ndiye ameitwa angeitikia wito huo haraka au laa, Utoh alisema kuwa ingetegemeana na kauli aliyoizungumza.

“‘Inge-depend’ na ‘statement’ ambayo nimeizungumza, nimeizungumza kwa madhumuni gani, kwahiyo ‘I can not say’ (siwezi kusema) kama ingekuwa ni mimi kwa sababu sijajua ‘exactly’ alichozungumza Profesa Assad,” alisema Utoh.

Alisema kuwa Bunge au ofisi ya CAG kuwa na meno au kutokuwa na meno inatokana na mtu anayesema hivyo kasimamia upande gani.

“Ni ‘issue’ tata kidogo, tunahitaji kuwa na busara sana katika ‘kuli-handle’ (kulishughulikia) hili, nimesema itumike busara kubwa katika ‘kuli-solve’ suala hili, suala la kwamba ilitumika au haijatumika hayo mimi sijasema,” alisema.

ZITTO KORTINI

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), jana aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akisema kuwa ameshauriana na wanasheria na wabunge wenzake na kuamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya kinga ya CAG.

 “Baada ya kushauriana na wanasheria na wabunge tumeona ni muhimu sana kwa maslahi mapana ya nchi yetu kulinda katiba yetu.

“Baadhi ya wabunge kutoka vyama vyote tumeamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya kinga ya CAG kwa mujibu wa katiba na mamlaka ya Spika kutoa wito kwa CAG.

 “Asasi za kiraia zinazojishughulisha na uwajibikaji naomba tuwaone katika suala hili la CAG. Ni jambo la hatari sana CAG kushughulikiwa namna hii. Sauti zenu ni muhimu sana.

 “Profesa Assad alifanya ukaguzi maalumu kuhusu matumizi ya Sh trilioni 1.5 zilizokuwa hazina maelezo kwenye ukaguzi wa mwaka 2016/17.  

“Taarifa hiyo ya ukaguzi maalumu ipo mezani kwa Spika na Spika ameikalia hajaipeleka PAC ili iwasilishwe bungeni. Mvutano huu wa Spika na CAG ni ujanja tu,” aliandika Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT- Wazalendo, alikwenda mbali katika ujumbe wake huo na kudai kuwa: “Hivi sasa Spika ameagiza Kamati za Bunge za kuisimamia Serikali (PAC, LAAC, Bajeti na Uwekezaji) kutofanya kazi na CAG wala maofisa wake. Hii maana yake ni kuwa Bunge halitajadili taarifa za PAC/LAAC kwenye mkutano ujao wa Bunge (kukwepa TZS 1.5T ). Hapa Spika anavunja katiba.

“Kuna mpango wa muda sasa kutaka kumwondoa Prof. Assad katika nafasi ya CAG kwa sababu ‘ana kiburi, misimamo mikali na hanyenyekei mamlaka ya juu’. Kikatiba wameshindwa. Walitaraji angetoka Septemba 2019, lakini kikatiba haondoki mpaka afike umri wa kustaafu. Wanatafuta njia.”

Aliendelea: “Ni nadra na haijapata kutokea kwenye Jumuiya ya Madola Spika wa Bunge na Mkaguzi Mkuu (CAG) wa nchi kuparurana namna hii. Bunge na Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa huwa upande mmoja wakati wote. Niwaambie Watanzania, Spika Ndugai kwenye hili anatumika na Rais kwa lengo la kuzuia jambo.”

Mwaka jana lilipoibuka suala la upotevu wa Sh trilioni 1.5 katika hesabu za Serikali mwaka wa fedha 2016-2017, Assad aliulizwa kuhusu nini kifanyike, akataka Bunge liulizwe kwani ndilo lenye kutakiwa kuibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha hizo.

SPIKA NDUGAI AJIBU

Kutokana na madai hayo ya Zitto kuhusu Kamati za Bunge kuagizwa kutofanya kazi na CAG, Spika Ndugai alimtaka mwandishi amuulize Zitto aeleze alipotoa habari hizo.

“Kwa kweli hilo muulizeni yeye mwenyewe, mimi niko Kongwa, nipo shambani kwangu. Wapo watu huzua mambo kila kukicha kila dakika na mmojawapo ni huyo (Zitto),” alisema Ndugai.

MDEE ANENA

Kwa upande wake, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), ambaye pia ametakiwa na Spika kuripoti kwenye kamati hiyo Januari 22, aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kuwa atakwenda mbele ya kamati hiyo huku akisisitiza kusimamia kile kilichosemwa na CAG.

KITUO CHA SHERIA

Kutokana na mnyukano huo, jana Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia kwa mkurugenzi wake Anna Henga, kilisema kuwa ofisi ya CAG imeundwa kikatiba kupitia ibara ya 143 na 144 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara.

Henga alisema; “lbara ya 143 (1) inaeleza kuwa kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano na kifungu cha (2) kinaeleza majukumu yake, ambayo ni kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa.

“Na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya katiba na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe

“Majukumu mengine kwa mujibu wa kifungu cha (2) ni kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yoke yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, ambazo zimetumika kwa ajili ya shughuli zilizohusika na matumizi ya fedha hizo.”

Alisema kifungu cha (3) kinaeleza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu na kila mtumishi wa Serikali aliyeruhusiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na haki ya kuchunguza vitabu, kumbukumbu, hati nyinginezo zote zinazohusika na hesabu za aina yoyote iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.

KAULI YA CAG

Desemba mwaka jana, Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

Katika majibu yake CAG alisema; “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge, kama tunatoa ripoti zinazoonesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika, ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

 “Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

Kutokana na mahojiano hayo, Spika Ndugai alisema kuwa kama CAG anasema Bunge ni dhaifu basi mpotoshaji mkubwa atakuwa yeye mwenyewe na wafanyakazi wake.

“Kwahiyo sasa na kwa mujibu wa kinga, madaraka na haki za Bunge kwa sheria za Tanzania na kwa mujibu wa mamlaka niliyonayo kama Spika, kifungu cha 4, kifungu kidogo cha kwanza (a) cha nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januari mwaka 2016.

“Suala hili nalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ili waweze kulifanyia kazi. Kwahiyo CAG Profesa Assad anapaswa kufika kwenye kamati Januari 21 mwezi huu, nakazia wito huu atokee tarehe 21 na ajitokeze kwenye kamati na kuthibitisha maneno yake ya huko Marekani,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles