Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali imezitaka taasisi zinazodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) zaidi ya Sh bilioni 20 kulipa madeni hayo haraka kurahisisha utoaji huduma.
MSD Kanda ya Mashariki ambayo inahudumia vituo 966 kwenye halmashauri 23 za Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Zanzibar inadai zaidi ya Sh bilioni 20 kutoka katika taasisi mbalimbali za umma.
Akizungumza Septemba 13,2023 wakati Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilipotembelea MSD, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amesema changamoto kubwa inasababishwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutolipa madai ya watoa huduma kwa wakati.
“MSD imeuza dawa inatakiwa ilipwe fedha lakini bima wanachelewesha fedha, hilo tutalisimamia kwa karibu na tutawaelekeza walifanyie kazi haraka.
“Mteja akishatoa huduma anatakiwa alipwe haraka, tulishaelekezwa na Rais kwamba ndani ya siku 60 mtoa huduma awe amelipwa, lakini hakuna sababu ya kufika siku 60…tutawasimamia,” amesema Dk. Mollel.
Kuhusu ushuru unaotozwa MSD kwa dawa na vifaa tiba vinavyopelekwa Wilaya ya Mafia mkoani Pwani, amesema watawasiliana na wizara husika kutatua changamoto hiyo.
“Ukitoza kodi kwenye dawa mfano unapeleka Mafia bei za dawa zitapanda zaidi ukilinganisha na wilaya zingine, tutalifanyia kazi mara moja hili ni suala la mawasiliano tu,” amesema.
Aidha ameziagiza halmashauri kukadiria dawa kulingana na mahitaji yaliyopo kwenye maeneo yao kuepuka kukosekana kwa dawa katika vituo vya afya.
“Tulikwenda Mbozi kwenye kituo cha afya wanalalamika hawana dawa, walikadiria watatumia dawa za Sh milioni 387 lakini mpaka siku wanayolalamika walikuwa wameshapewa dawa za Sh milioni 459.
“Waganga wakuu wa wilaya na mikoa wahakikishe wanapokwenda kwenye bajeti wakadirie dawa kulingana na magonjwa ya maeneo husika.
“Najua kuna magonjwa yanayotokea ambayo hayajapangwa, tuna namna ya kushughulika nayo lakini yale yaliyozoeleka wakadirie kwa thamani halisi.
“Wilaya hiyo hiyo wananchi wanalalamika hakuna dawa lakini tukakuta wana zaidi ya Sh milioni 300 kwenye akaunti kwa miezi mitatu na hakuna dawa iliyonunuliwa,” amesema Dk. Mollel.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema wanaendelea kufanya maboresho mbalimbali ambapo wanajivunia kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa hasa vifaa tiba.
“Kwa sasa tunaongelea utekelezaji wa mikakati ambayo tuliiweka, tumeboresha mikataba, uagizaji, tunaboresha miundombinu tunajenga maghala mawili; Mtwara limeanza na Dar es Salaam ni moja ya mipango kwenye kujenga maghala mapya,” amesema Tukai.
Meneja wa MSD Kanda ya Mashariki, Betia Kaema, amesema moja ya changamoto inayowakabili ni madeni wanayodai katika vituo mbalimbali hatua ambayo inaweza kuathiri utoaji huduma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo, amesema wameridhishwa na maboresho yanayoeendelea katika bohari hiyo hasa upatikanaji wa dawa.
“Tumejifunza mambo mengi, tumefurahi kuona jinsi bohari kuu ya dawa inavyofanya kazi, tumeona jinsi ilivyojipanga kimikakati kuzalisha dawa,” amesema Nyongo.
Kamati hiyo pia imeitaka NHIF kulipa madeni kwa wakati ili hospitali zinazodaiwa ziweze kulipa madeni MSD.
“Mantiki ya Bunge kukubali MSD aongezewe mtaji ni katika kutatua changamoto hii kwa sababu anapokuwa na mtaji mdogo halafu akajikuta anadai madeni inakuwa ni tatizo kubwa katika kufanya kazi kwa ufanisi.
“Tutaongea na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya waweze kulipa madeni ili MSD iendelee na kazi zake za kupelea dawa kwa wakati,” amesema.