27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MNANGAGWA AMTEUA MWAMUNYANGE KUCHUNGUZA VURUGU ZIMBABWE

HARARE, ZIMBABWE


MKUU wa majeshi mstaafu nchini Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, ameteuliwa na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa kuwa mjumbe wa tume ya watu saba itakayochunguza vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu nchini hapa.

Rais aliyeongoza kwa muda mfupi Afrika Kusini, Septemba 2008 hadi Mei 2009, Kgalema Motlanthe, ataongoza tume hiyo inayotarajiwa kumaliza kazi yake ndani ya miezi mitatu.

Tume hiyo inatarajiwa kuchunguza kiini cha vurugu hizo, ambazo zilisababisha vifo vya watu sita baada ya wanajeshi kuzima maandamano ya wapinzani siku mbili baada ya uchaguzi wa Julai 30.

Wakati wa maandamano hayo ya wafuasi wa upinzani mjini hapa, yaliyofuatia tangazo la Tume ya Uchaguzi kuwa chama tawala cha ZANU-PF kimeshinda viti vingi, askari walirusha risasi za moto kuwatawanya.

Uchaguzi huo ambao umehalalisha urais wa Mnangagwa, ulitazamiwa kuwa ni mwanzo mpya wa siasa za kidemokrasia tangu kung’olewa madarakani kwa Robert Mugabe Novemba 2017.

Hata hivyo, kuingia kwa jeshi mitaani na kuwafyatulia risasi waandamanaji, kulizusha shaka juu ya mustakabali wa Zimbabwe.

Swali kuu zaidi ni kuwa wengi wametaka kujua nani hasa aliwaamuru wanajeshi kuzuia maandamano hayo, kitu ambacho tangu awali kilimfanya Mnangagwa aape kukitafutia jibu.

Jenerali Mwamunyange ambaye alikuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 10, kuanzia 2007 hadi alipostaafu 2017, ndiye mtu pekee katika tume hiyo mwenye usuli wa mambo ya kijeshi.

Mwanasheria kutoka Uingereza, Rodney Dixon ambaye aliiwakilisha Serikali ya Kenya katika kesi ya vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) pia ni mmoja wa wajumbe wa tume hiyo.

Mjumbe mwengine kutoka nje ya Zimbabwe ni Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyaoku kutoka Nigeria.

Kutoka ndani ya Zimbabwe, wajumbe ni Profesa Lovemore Madhuku kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe, Profesa Charity Manyeruke na Vimbai Nyemba ambaye ni rais wa zamani wa chama cha wanasheria wa Zimbabwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles