30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mloganzila kutoa mawe kwenye figo kwa kutumia miozi

Aveline Kitomary -Dar es salaam

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila, inatarajia kuanza kutoa huduma ya kuondoa mawe kwenye figo kwa njia ya kisasa ya kutumia miozi.

Huduma nyingine inayotarajiwa kutolewa mapema Februari ni upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant) kwa wagonjwa wa saratani, huduma ambayo itakuwa ya kwanza kutolewa nchini.

Akizungumza jana katika kampeni ya ‘tumeboresha sekta ya afya’ inayofanywa na taasisi mbalimbali za afya  nchini, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Julieth Magandi alisema tayari wameshaandaa wataalamu kutokana na huduma hizo kuwa na uhitaji mkubwa.

 “Kwa mwaka wa fedha 2019/20 Serikali imetenga Sh bilioni 8 kwa ajili ya uanzishwaji wa kituo cha umahiri cha upandikizaji viungo (Centre of Excellence for organ Transplant) katika eneo la Mloganzila, huduma kama ya macho, upandikizaji figo, ini, mimba zitapatikana hapo.

“Tunaendelea kuboresha huduma zetu kama huduma za wagonjwa mahututi (ICU) ambapo tunategemea kupokea wataalamu sita kutoka nchi ya Cuba, hao wamebobea katika huduma za ICU, vilevile taasisi inaendelea kudhamini mafunzo ya kibingwa kwa watumishi wake kwani mpaka sasa tumedhamini watumishi 45.

 “Mipango yetu ni kuendeleza uhusiano na taasisi za ndani na nje ya nchi, ikiwemo Chuo Kikuu cha Yonsei cha Korea na zingine. Pia tumeandaa mpango mkakati wa mwaka 2020-2025 utakaoonyesha dira ya hospitali na utekelezaji wa huduma zote ,” alieleza Dk. Magandi.

Aidha Dk. Magandi alisema utoaji wa huduma nzuri umeweza kufanya wagonjwa kuendelea kuongezeka hospitalini hapo.

 “Tangu Julai hadi Septemba wagonjwa walikuwa 17,116  na kwa Oktoba hadi Desemba mwaka jana wamefikia 24,945 sawa na asilimia 46. Hawa ni wagonjwa wa ndani.

“Kwa wagonjwa wa nje, robo ya Julai hadi Septemba  mwaka 2018 walikuwa 1,459 na kwa robo ya mwaka 2019 kuanzia Oktoba hadi Desemba walikuwa 2,419 sawa na asilimia 66,” alibainisha Dk. Magandi.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mine, alisema hospitali hiyo imefanikiwa kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear Implant), kufanya upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo (Celebral aneurysms) na upasuaji wa matatizo ya mgongo (Spinal Surgery).

“Katika kipindi cha Oktoba mwaka 2019 jumla ya watoto watatu walipandikiziwa vifaa vya kusikia. Kati ya hao, wawili ni Watanzania na mmoja alitokea nchi ya Rwanda.

“Gharama ya upasuaji kwa mgonjwa mmoja ni Sh milioni 36 wangeenda nje ya nchi ingetumika Sh nilioni 80 mpaka 100 kwa mtoto mmoja, hivyo kwa upasuaji huu tumeokoa kiasi cha Sh milioni 200 endapo wangepelekwa nje.

 “Huduma nyingine ya kibingwa ni upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo. Hospitali hii ni ya pili kutoa huduma hiyo baada ya Moi.

“Hadi kufika Novemba 12 mwaka jana jumla ya wagonjwa watano wamefanyiwa upasuaji huo na gharama kwa mgonjwa mmoja ni Sh milioni 20, endapo angefanyiwa nje ya nchi ingegharimu Sh milioni 40,” alisema. Dk Magandi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles