28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MLOGANZILA KUCHUJA DAMU WAGONJWA WA FIGO


Na Veronica Romwald-Dar es Salaam    |

SERIKALI imeongeza kituo kipya cha huduma ya uchujaji damu (dialysis) kwa wagonjwa wa figo katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila (MAMC).

Huduma hiyo ilizinduliwa rasmi jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya na wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo.

Hatua hiyo inafanya Tanzania kuwa na vituo saba vya umma vinavyotoa huduma hiyo kwa wagonjwa hao.

Vingine ni Benjamin Mkapa (Dodoma), Hospitali ya Taifa Muhimbili (Dar es Salaam), Hospitali ya Bugando (Mwanza), Hospitali ya KCMC (Kilimanjaro), Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Mnazi Mmoja (Zanzibar).

Akizungumza jana, Dk. Ulisubisya alisema kituo hicho kimewekwa mashine 12 na kitakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 10,000 kwa mwaka.

“Wakiwamo wasio na maambukizi na wenye maambukizi, kinachoongozwa na madaktari bingwa wazoefu na wauguzi wenye ari, kitakuwa kituo-darasa cha tiba makini kwa wagonjwa wote.

“Vile vile kituo hiki kitatoa mafunzo endelevu kwa madaktari wajao na kitakuwa chachu ya utafiti wenye kutoa miongozo ya matibabu na kuboresha sera za matibabu ya wagonjwa ya figo nchini,” alisema.

Kuhusu tuhuma za wagonjwa wengi kufariki dunia hospitalini hapo wakati wakisubiri huduma, Dk. Ulisubisya alisema madai hayo hayana ukweli wowote.

“Wagonjwa wanapoletwa hospitalini tunawatibu lakini hatuwezi kuzuia kifo, wapo ambao hufariki dunia lakini si kwa wingi unaoelezwa,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo alisema kwa miezi sita hadi sasa tangu kuzinduliwa kwa MAMC, wanafunzi 350 wamepata mafunzo mbalimbali ya udaktari na udaktari bingwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles