Mlinzi awafungia walimu ofisini

ndalichakoNa RAMADHAN HASSAN, DODOMA

MLINZI wa Shule ya Msingi Medeli iliyopo katika Manispaa ya Dodoma, Zebedayo Bendera, amewafungia ofisini baadhi ya walimu wa shule hiyo baada ya kushindwa kumlipa mshahara wake.

Wakati Bendera anafunga ofisi hiyo jana asubuhi, ofisini walikuwamo walimu kadhaa pamoja na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Rehema William.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika shuleni hapo jana, mlinzi huyo alisema aliamua kuchuku uamuzi huo baada ya walimu hao kushindwa kumlipa mshahara kuanzia Januari mwaka huu.

“Mshahara wangu ni shilingi 70,000 kwa mwezi na kwa kuwa sijalipwa kwa miezi saba, nawadai shilingi 490,000.

“Kwa hiyo, nimeamua kuwafungia ndani ili kuwashinikiza wanilipe fedha zangu kwa sababu hawataki kunilipa kwa makusudi kwani fedha wanazo.

“Kitendo cha hawa walimu kutonilipa mshahara kimeathiri maisha yangu na familia yangu kwa sababu sina kazi nyingine ya kufanya zaidi ya huu ulinzi.

“Kwa hiyo, nitaendelea kuwafungia ofisini hadi nitakapolipwa mshahara wangu maana hii siyo mara ya kwanza kuwafanyia hivi.

“Hata mwezi uliopita mimi na mlinzi mwenzangu tuliwafanyia hivi, wakaita polisi wakaja kutukamata na mwishowe wakatulipa 50,000 na kuachiwa,” alisema Bendera.

Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Mkuu  Rehema alisema hiyo ni mara ya nne mlinzi huyo kuwafungia ofisini.

“Ni kweli huyo mlinzi anatudai kwani hesabu zinaonesha yeye na mwenzake wanatudai zaidi ya shilingi laki tatu kila mmoja.

“Siyo kwamba hatutaki kuwalipa bali tunashindwa kufanya hivyo kwa sababu Serikali haileti fungu la walinzi kwenye fedha zinazopelekwa mashuleni,” alilaalmika Mwalimu Rehema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here