30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MLEZI WA MAPACHA WALIOFARIKI AIBUKA

Na WAANDISHI WETU-IRINGA/DAR      |     


MLEZI aliyewalea mapacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti, ameibuka na kusimulia namna alivyoachishwa kazi ya usafi hospitali ili aweze kuwalea.

Amesema kwa kipindi chote cha miaka saba alichowalea tangu walipozaliwa, hajawahi kukutana na ndugu yao yeyote zaidi ya kusaidiwa na kanisa.

Akizungumza jana mjini hapa, mlezi huyo, Betina Mbilinyi (52), mkazi wa Ikonda, Wilaya ya Makete mkoani Njombe, alisema tangu alipopewa jukumu la kuwalea mapacha hao na Shirika la Misheni, kwa miaka saba aliishi nao ingawa walikuwa na uwezo mkubwa tangu wakiwa wadogo.

“Huu ni msiba wa watoto wangu, umeniumiza. Niliwalea Maria na Consolata tangu walipozaliwa hadi walipofikia umri wa miaka saba.

“Hatua ya kuwalea ilitokana na uongozi wa Hospitali ya Misheni Ikonda, kunikabidhi na awali pale nilikuwa ni mfanyakazi wa usafi.

“Ila baada ya tu ya kuzaliwa na kukabidhiwa jukumu hili, niliachishwa kazi yangu ya awali na muda wote nikawa nalea hao watoto.

“Kwa kipindi chote niliokaa nao, sijapata kumuona ndugu yeyote wa hawa watoto, ila nilisikia alipata kuja baba yao mkubwa akitokea mkoani Mbeya.

“Sikuweza kukutana naye kwani wakati amekuja nyumbani, mimi nilikuwa shamba na niliambiwa tu. Ila kwa upande wa mama yao, ndugu walikuwa wakija zaidi ya mara mbili,” alisema Betina.

Alisema uongozi wa Hospitali ya Ikonda ilimwomba awalee watoto hao kwa kuwa alikuwa akiishi jirani na hospitali hiyo.

“Maria na Consolata walizaliwa mazingira ya misheni, hivyo  ilikuwa rahisi kwangu kuwapeleka hospitali pale  walipohitajika na kuwarudisha nyumbani kwangu. Na wakati nawaleta nami nilikuwa na watoto wawili,” alisema.

Betina alisema aliwapenda sana Maria na Consolata  kutokana na kuwa na heshima na wasikivu kwa kila jambo  wanaloelezwa na kwamba walipendana na watoto wake ambao nao waliwaona ni ndugu wa kuzaliwa nao.

“Pamoja na kuishi nao kama familia yangu ila nilikuwa  nikilipwa mshahara na Misheni, ni mshahara ule ambao nilikuwa nikilipwa kwa kazi yangu ya usafi hospitali.

“Nilifurahia kuifanya kazi hii ya kuwalea Maria na Consolata kwa kujituma na kuwapa upendo unaostahili wakati wote,” alisema Betina.

CHANGAMOTO YA ULEZI

Akizungumzia changamoto namna alivyowalea Maria na Consolata, alisema awali wakiwa watoto wachanga kazi ilikuwa ngumu, lakini kadiri walivyokuwa wanakua, ilikuwa rahisi kwake.

“Awali nilikuwa nikiiona ngumu, lakini baada ya muda nilikuwa nimeizoea na kuona ni jambo la kawaida kwani nilihisi ni watoto wangu wa kuwazaa.

“Mshahara wangu ulikuwa ni uleule ambao nilikuwa nikilipwa, japo siwezi kuutaja hapa ila ni mshahara ulionifaa na ndio ambao nalipwa hadi sasa,” alisema.

KIPAJI CHAO

Betina alisema baada ya kukaa na mapacha hao kwa miaka saba, walianza darasa la kwanza na walipofaulu walijiunga na elimu ya sekondari na kulazimika kuondoka wilayani Makete kwenda Kilolo naye alirudishwa katika kazi yake ya usafi.

Alisema kwa kuwa Maria na Consolata, walikuwa ni sehemu ya familia yake, hata wakati wa likizo walikuwa wakirudi nyumbani kwake Makete kwa mapumziko.

“Mara yao ya mwisho ambayo sitaisahau, walikuja Agosti mwaka jana na hii ndio ilikuwa likizo yao ya mwisho na tuliongea nao mambo mbalimbali, na kila ninapoyakumbuka baadhi ya malengo yao ya mbeleni, najisikia natokwa na machozi.

“Ndoto kubwa ilikuwa ni kumaliza chuo na kuja kufanya kazi itakayowapatia kipato ambacho wataniwezesha na  mimi na familia yangu. ‘Tunaomba mama tuombee tuwe wazima, tukimaliza chuo tutakulea na wewe mama…’, hii ndiyo ilikuwa kauli yao ya mwisho kwangu,” alisema Betina.

MKUU WA SHULE

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Maria Consolata iliyopo Kilolo mkoani Iringa, Jefrod Kipindi, alisema hakuamini taarifa za mapacha hao kufariki dunia ila baada ya kuona salamu za rambirambi za Rais John Magufuli, ilimfanya aamini.

Alisema aliwapokea Maria na Consolata Januari 2011 wakitokea Ikonda wilayani Makete na ameishi nao kwa miaka saba wakiwa shuleni hapo.

Mwalimu Kipindi, alisema pamoja na kujiunga na kidato cha sita Shule ya Sekondari Udzungwa, bado makazi yao yaliendelea kuwa shuleni hapo katika nyumba yao ya Nyota ya Asubuhi.

Alisema kati ya wanafunzi zaidi ya 163 waliokuwapo wakati wakijiunga na kidato cha kwanza mwaka 2011, Maria na Consolata walikuwa ni wanafunzi wa kipekee kwani mbali ya hali waliyokuwa nayo, walikuwa ni wanafunzi watiifu na wachangamfu.

“Awali wanafunzi hao walikuwa wakijaza watu shuleni na mitaani walikokuwa wakipita, hasa wanapokwenda kanisani, kila mtu alikuwa akiwasogelea na kuwashangaa sana ila baada ya kuzoeleka hakuna aliyewashangaa, waliwachukulia kawaida.  ilikuwa nikiamini ndoto yao itatimia, ila msiba wao umetushtua sana,” alisema Kipindi.

Kaka wa mapacha hao, David Mwakikuti, alisema kifo chao kimempa funzo kubwa katika maisha yake hapa duniani, kwani hajawahi kuona watu wanaojiamini na kusimamia haki kama walivyofanya enzi za uhai wao.

“Waliniambia kuwa nitakapokuwa vizuri kiuchumi basi nisiache kumtegemea Mungu na niamini katika kile ninachokiamini na kukubaliana na hali halisi ya maisha halisi tuishiyo hapa duniani, hivyo nitaendelea kuwajali watu wote na waina zote,” alisema Mwakikuti.

MAMA MKUBWA

Mama mkubwa wa watoto hao, Anna Mushumbushi, alisema familia walikuwa bega kwa bega katika kuwasaidia watoto hao tangu walipozaliwa na wala hawakuwatenga kama baadhi ya wanavyodai.

Alisema taarifa za mapacha hao kuzaliwa alizipata kupitia vyombo vya habari baada ya siku saba tangu kuzaliwa kwao na ndipo alipofunga safari kwenda Makete kuwaona na tayari walikuwa wameshakabidhiwa masista wa Shirika la Misheni kuwalea.

“Baada ya baba wa watoto hao kufariki dunia, ilibidi baadhi ya watoto akiwemo kaka yao na Editha (dada yao) waliwachukua na kwenda nao nyumbani Bukoba kwa babu yao na bibi yao na waliwasaidia kwa hali na mali,” alisema.

TARATIBU ZA MAZISHI

Akitoa utaratibu wa shughuli za mazishi za mapacha hao kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, alisema yatafanyika kesho kwenye makaburi ya viongozi wa Kanisa la Romani Katoliki.

Alisema viongozi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki msiba huo.

Maria na Consolata walizaliwa mwaka 1996 katika   Hospitali ya Misheni Ikonda, Kijiji cha Ikonda, Wilaya ya Makete mkoani Njombe.

Walifariki dunia juzi usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa wakiwa katika matibabu.

MADAKTARI

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kifua na Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Paulina Charles, alisema tatizo la upumuaji lililokuwa likiwasumbua, lilitokana na ulemavu wa maumbile katika sehemu ya kifua.

Alisema waliwapokea mapacha hao Februari 3, mwaka huu, wakitokea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa wakiwa na shida katika mfumo wa hewa.

“Ikabidi tuwapeleke ICU kwa uangalizi zaidi na uchunguzi kujua nini hasa kilisababisha kupata tatizo katika njia ya mfumo wa hewa,” alisema.

Alisema taarifa za awali zilieleza walikuwa wamepata maambukizi ya bakteria, hivyo katika uchunguzi wao  walitaka kujua zaidi ni aina gani ya bakteria ambao walikuwa wamewashambulia.

Paulina alisema walichukua sampuli za makohozi yao wakayaotesha kitaalamu na hatimaye waliweza kuwabaini bakteria waliowashambulia.

Alisema waliwapa dawa sahihi walizotumia kwa wiki mbili kwa njia ya sindano ambayo ilikwenda kuwaua bakteria husika.

Bingwa huyo alisema waliwaita walezi wao wakakaa kikao na kuchukua taarifa ya historia ya maisha yao, ambayo ilionyesha tangu walipozaliwa walikuwa na upumuaji hafifu.

“Tulitumia kipimo cha kiwango cha juu cha CT scan katika uchunguzi. Awamu hii tuliangalia mfumo wa homoni, kifua na uti wa mgongo na matokeo yalionyesha walikuwa na ulemavu wa maumbile ya kifua na yalihusisha mifupa ya uti wa mgongo,” alisema.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake Muhimbili, Vincent Tarimo, alisema mapacha hao walikuwa wanashirikiana katika mfumo wa njia ya chakula.

“Walikuwa wanashirikiana ini, utumbo mdogo kuna mahali fulani ulikuwa umeungana, ndiyo maana walikuwa pia na njia moja ya haja kubwa,” alisema.

Alisema walikuwa na miguu mitatu na miwili ndiyo ilikuwa mikubwa na yenye nguvu kuliko ule wa tatu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, alisema amepokea taarifa za kifo cha mapacha hao kwa masikitiko makubwa.

“Waliletwa hapa JKCI wakisumbuliwa na tatizo la nimonia, tulilitibu na likaisha, kisha tukawahamishia Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, walikuwa wamezaliwa kila mmoja akiwa na moyo wake. Lakini mmoja moyo wake ulikuwa upo upande wa kushoto kama unavyopaswa na mwingine ulikuwa upande wa kulia,” alisema.

Alisema mapacha hao walidumu kuishi kwa muda mrefu kwani walikuwa na afya njema.

HABARI HII IMEANDALIWA NA RAYMOND MINJA, FRANCIS GODWIN (IRINGA), NA VERONICA ROMWALD (DAR ES SALAAM)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles