24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Mlemavu afungiwa ndani miaka 11

Mtoto Mbeya
Fredrick Emmanuel

Na PENDO FUNDISHA – MBEYA

WASWAHILI wanasema ukistajabu ya Musa utaona ya Firauni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mtoto mwenye ulemavu kufungiwa ndani ya nyumba kwa miaka 11 na wazazi wake.

Tukio hili la kusikitisha lililotokea eneo la Mwambenja, Kata ya Ilemi mkoani Mbeya, limefanywa na wazazi wa mtoto huyo, kwa madai ya kuficha aibu kwa jamii.

Kwa kawaida binadamu hawezi kuishi ndani siku zote hizo, lazima atoke nje apate hewa na jua la asubuhi lenye vitamini D kwa ajili ya maendeleo ya afya yake.

Lakini mtoto huyo, Fredrick Emmanuel, ambaye sasa ana miaka 20, amekuwa akiishi ndani bila kutolewa nje, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kudhohofika kiafya.

Licha ya baadhi ya viongozi wa mtaa, majirani na marafiki wa karibu wa familia hiyo kupata taarifa hizo, hawakuchukua hatua yoyote kwa kipindi chote hicho.

Badala yake, wamewalalamikia wazazi na walezi wa kijana huyo kwa kushindwa kuweka wazi yaliyowasibu ili jamii iwasaidie.

Licha ya motto huyo kuzaliwa akiwa na ulemavu wa viungo vya mikono na miguu, pia ana utindio wa ubongo, hali inayomfanya kushindwa kuongea.

Pamoja na wazazi wake kujitetea kuwa wamekuwa wakimhangaikia kimatibabu kwa zaidi ya miaka 19, inaonekana wamekata tamaa na kuamua kumweka ndani, kisha kumwachia Mungu kama wanavyosema wenyewe.

Baba mzazi wa kijana huyo, Emannuel John, aliliambia MTANZANIA juzi nyumbani kwake  Mtaa wa Mwambenja kuwa Fredrick alizaliwa mwaka 2007, ukiwa ni uzao wake wa kwanza katika familia hiyo.

Alisema wadogo zake watatu wamezaliwa wakiwa wazima na wenye afya njema.

“Mwanangu alizaliwa akiwa tayari na ulemavu wa viungo na utindio wa akili, tulihangaika naye mno kutafuta matibabu ambayo yangemsaidia awe vizuri, lakini jitihada ziligonga mwamba.

“Baada ya jitihada zote za hospitali kufanyika, ilinilazimu kuingia kwa waganga wa tiba asili, ambako huko nilihangaika bila ya kupata ufumbuzi, nikaamua kuachana nao na kumwachia Mungu mwenyewe,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwambenja, Rosemary Jama, alisema taarifa za Fredrick kuishi ndani ya nyumba hiyo walikuwa nazo, lakini hawakuwahi kupata taarifa kama hatolewi nje.

“Sisi tunafahamu ndani ya nyumba ya Emmanuel, kuna mtoto ambaye ni mlemavu, hatukufahamu mazingira anayoishi, nimejionea kweli huu ni unyanyasaji wa kijinsia, mtoto anaonekana hapati chakula kama inavyotakiwa,” alisema.

BABA AKAMATWA

Baada ya kupatikana taarifa hizo, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, juzi limemkamata baba wa kijana huyo.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Mbeya, Ofisa wa Polisi Janet Masangano, alisema baba mzazi wa kijana huyo, Emmanuel John, anashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kufuatia tuhuma zinazomkabili za kumficha mtoto wake ndani kwa zaidi ya miaka 11 kwa madai ya kuficha aibu.

“Asilimia hamsini ya Watanzania ni watoto. Kila mtoto ni hazina. Kila mmoja ana thamani kwa familia yake, kwa jamii yake na taifa kwa

ujumla. Sote tunalo jukumu la kutekeleza, hivyo kitendo kilichofanywa na wazazi wa kijana huyu, ni ukiukwaji wa sheria na haki za watoto kama zinavyoelekeza,” alisema.

Alisema sheria ya mtoto iliyopitishwa na Serikali mwaka wa 2009, huwalinda watoto dhidi ya mazingira hatarishi na unyanyasaji, na kwamba kama kila mtu mzima akilea mtoto mmoja, watoto (wote) wa Tanzania watakuwa katika mazingira salama.

“Kijana huyu, alizaliwa na ulemavu wa viungo, lakini kwa jinsi tunavyomuona, inaonekana wazazi hawakumtendea haki na kumsababishia madhara makubwa ya kiafya hali iliyopelekea mtoto huyo kushindwa kuongea kutokana na kumfungia ndani,” alisema.

Alisema maelezo ya awali ya wazazi wa kijana huyo, yameweka bayana kwamba walezi hao baada ya kumuhangaikia kwa muda mrefu bila kupata nafuu, sasa wameamua kumtelekeza na kuamua kumfungia ndani na kumwachia Mungu kama walivyoeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles