23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkwasa ataja sababu za kumuita Kazimoto

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya soka ‘Taifa Stars’, Boniface Mkwasa, amesema uwezo mkubwa aliokuwa nao kiungo wa Simba, kazimotoz, ndio umemfanya amuite kwenye kikosi chake kitakachocheza na Chad, Machi 23 kwenye mchezo wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), utakaochezwa mji wa Djamena, nchini Chad.

Mkwasa alimjumuisha mchezaji huyo kwenye kikosi chake hicho chenye jumla ya wachezaji 25, licha ya kuwa tayari ameshatangaza kuacha kuichezea timu ya Taifa ili kutoa nafasi kwa wachezaji wengine.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkwasa alisema, Mwinyi ameonyesha mchango mkubwa kwenye timu yake ya Simba na ndio sababu iliyompelekea kumjumuisha kwenye kikosi chake ambacho kulingana na ratiba ilivyobana anahitaji kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa ili kuweza kupambana na Chad kwani hawana muda mrefu wa kujiandaa.

“Hizo taarifa za kuwa amestaafu kuichezea timu ya Taifa sijazipata hivyo haikuwa kikwazo kwangu kumuita, lakini pia bado ana kiwango kizuri ni kijana mkongwe na amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu yake, bado ana nafasi kubwa ya kulisaidia Taifa lake,” alisema.

Akizungumzia utovu wa nidhamu aliouonyesha Mwinyi wiki chache zilizopita kwa kumpiga mwandishi wa habari Shinyanga, Mkwasa alisema kama anatuhumiwa kwa vitendo vingine vya utovu wa nidhamu hajawahi kuvionyesha akiwa uwanjani, hivyo hana kikwazo chochote cha kumfanya asimuite kwenye kikosi chake.

“Kama alionyesha utovu wa nidhamu ni nje ya uwanja, nina imani watakaa watazungumza na yataisha kwa amani,” alisema.

Katika hatua nyingine, MTANZANIA limebaini chanzo cha kutemwa kwa winga wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Ngassa, katika kikosi cha Stars ambacho kitavaana na Chad mwezi huu.

Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zinadai kuwa Ngassa ambaye anaichezea klabu ya Free State ya Afrika Kusini, amefanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kushoto juzi, baada ya kuumia vibaya na atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili au zaidi.

Mkwasa alitangaza kikosi cha wachezaji 25 juzi huku akimtema Ngassa kutokana na matatizo aliyopata pamoja na nyota wengine ambao hawapo fiti kwa ajili ya kuivaa Chad Machi 23, mwaka huu ugenini.

Imeelezwa kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilikuwa tayari limetuma barua kwa klabu ya Free State kwa ajili ya kumuombea ruhusa ya kujiunga na Stars, lakini ikashindikana kutokana na winga huyo kuwa majeruhi.

Kwa sasa Free State inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 28.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles