WASWAHILI wana msemo wao, “Wapiganapo mafahari wawili ziumiazo ni nyasi”.
Msemo huu unatumiwa sana na wananchi walio wengi hapa Zanzibar, wakisema kuwa yanapotokezea machafuko katika nchi waathirika wakubwa ni watu wa hali ya chini.
Ikiwa ni takribani miezi mitano imepita tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, kwa madai ya kuwapo kwa dosari nyingi, hali hiyo imesababisha kuzuka hofu si tu kwa wananchi wa Zanzibar bali hata raia kutoka mataifa mengine ambao wamekuwa wakija na kuvitembelea visiwa hivi mara kwa mara.
Tayari tume hiyo imeshatangaza upya tarehe ya kurejewa kwa uchaguzi huo ambao utafanyika Machi 20 mwaka huu.
Kufuatia hali hiyo, wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakiendelea kukumbana na hali ngumu ya maisha inayotokana na kuongezeka kwa mfumko wa bei kwa bidhaa muhimu za vyakula.
Ripoti kutoka kitengo cha takwimu za bei Zanzibar iliyo chini ya ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, inaonesha kuwa mfumko wa bei visiwani Zanzibar umezidi kuongezeka tangu kuanza kwa mkwamo wa kisiasa uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo cha Mfumko wa bei, Khamis Ahmada Shauri, Desemba mwaka jana mfumko wa bei uliongezeka na kufikia asilimia 11.7 ukilinganisha na asilimia 10.9 kwa mwezi Novemba 2015.
Aidha, anaongeza kuwa mfumko wa bei kwa bidhaa za chakula kwa mwezi wa Desemba 2015 uliongezeka na kufikia asilimia 18.1 ukilinganisha na asilimia 16.4 kwa mwezi wa Novemba, 2015.
Ongezeko hili linamaanisha kwamba kasi ya kupandakwa bei za bidhaa mbalimbali pamoja na huduma kwa mwaka ulioishia Desemba 2015 imeendelea kuongezeka ukilinganisha na kasi iliyokuwapo Novemba, 2015.
Kasi ya ongezeko hilo haikuishia hapo kwani katika mwezi wa Januari na Februari hali ya mfumko wa bei iliongezeka tena na kuwafanya wananchi wengi kuendelea kusakamwa na hali ngumu ya maisha na wengine kushindwa kumudu milo mitatu kwa siku.
Kulingana na Kitengo cha Takwimu za bei Zanzibar, mfumko wa bei kwa bidhaa za vyakula umeongezeka hadi kufikia asilimia 15.2 kwa mwezi Februari ikilinganishwa na asilimia 12.5 kwa mwezi Januari, 2016.
Katika kile kilichoonekana kushangaza wengi, Serikali kupitia kitengo hicho cha takwimu imesema kuwa ongezeko hilo la mfumko wa bei kwa kila mwezi halina uhusiano wowote na masuala ya kisiasa na uchumi.
Mtaalamu wa uchumi
Mtaalamu na Mchambuzi wa masuala ya uchumi visiwani Zanzibar, Dk. Mohammed Hafidh, anasema ukuaji wa uchumi katika nchi ni lazima uonekane katika maisha ya watu kwa kuzibadilisha hali zao mbaya za maisha na kuja kwenye maisha nafuu.
“Kukua kwa uchumi wetu kulipaswa kuonekane kwenye maisha ya watu. Tunataka uchumi wa nchi yetu ukue lakini pia mgawanyo wa taifa uangalie kwa wananchi wenye kipato cha chini, vinginevyo tutakuwa tunasema uchumi wetu umekuwa lakini hali kwa wananchi itabaki kuwa ngumu,” anasema.
Anasema mkwamo wa kisiasa unaoendelea hivi sasa umekuwa ni tatizo kubwa katika kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Anasema kuongezeka kwa mfumko wa bei kwa bidhaa muhimu kumetokana na wafanyabiashara wengi kuacha kuingiza bidhaa zao nchini pamoja na watalii wengi kusitisha safari zao za kuja Zanzibar.
“Mkwamo wa kisiasa umeleta athari kubwa kwa uchumi wa Zanzibar, hebu angalia uchumi wetu unategemea sana sekta ya utalii, lakini leo hii watalii wengi wamesitisha safari zao na wafanyabiashara wanaogopa kuingiza bidhaa zao kutokana na hali hii” anasema.
Hata hivyo anaishauri Serikali kuboresha maeneo muhimu kama vile michezo, elimu, afya, miundombinu na maji safi ili kuwawezesha wananchi kujikita zaidi katika shughuli zao za kiuchumi na kujiletea maendeleo.
MTANZANIA pia iliamua kuwatafuta baadhi ya wafanyabiashara ili kubaini chanzo cha kupandisha bidhaa zao.
Wafanyabiashara
Wafanyabiashara hao wanasema bidhaa nyingi zimepungua kuingia nchini jambo linalosababisha kununua na kuuza kwa bei ya juu ili wasipate hasara.
“Unajua sisi tunanunua bidhaa lakini tangu haya mambo ya kisiasa yatokee hapa kwetu wafanyabiashara wengi wamesita kuingiza bidhaa zao kwa kuhofia machafuko, na ndiyo maana sisi tunanunua kwa bei ya juu na tunauza kwa bei ya juu ili tupate faida,” anasema Ridhiwani Bakari, muuzaji wa duka la vyakula mjini Unguja.
“Bidhaa nyingi imekuwa ni vigumu sana kupatikana kwa hivi sasa, maana wafanyabiashara wakubwa ambao ndiyo tunaokwenda kununua kwao wameacha kufanya biashara kwanza kutokana na hii sintofahamu ya kisiasa iliyopo, kwa hivyo zile bidhaa zilizobaki tunauziwa kwa bei ya juu sana,” anasema mfanyabiashara mwingine Mbarouk Makame.
Wakati hali ya mfumko wa bei ikiendelea kuongezeka kila uchao, wananchi wamejitokeza kuiomba serikali kuchukua jitihada za ziada ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Tunaomba Serikali itusaidie kwa sababu hali inazidi kuwa ngumu na tunaoumia ni sisi wanyonge, viongozi wao hawana wasiwasi,” anasema Jamila Ali.