29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mkuu wa shule azungumzia ujauzito kwa wanafunzi

Ramadhan hassan – Dodoma

MKUU wa Shule ya Sekondari Dodoma, Amani Mfaume, amesema hakuna mwanafunzi ambaye atapata mimba katika shule hiyo na kuendelea na masomo.

Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa ambayo imekuwa ikisambazwa katika makundi ya WhatsApp kwamba kuna wanafunzi nane katika shule hiyo wamepewa ujauzito.

Akizungumza na MTANZANIA juzi jijini hapa, Mfaume alisema suala la wanafunzi kupewa mimba huwa linatokea mara moja moja, lakini wanaotakiwa kutoa taarifa ni Ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma.

Alisema taarifa za wanafunzi nane kupewa mimba si za kweli, na kwamba utaratibu wao kama mwanafunzi amepata ujauzito, ni kupelekwa nyumbani moja kwa moja.

“Wanapata mimba kwa sababu hatukai nao muda wote, mfano walikuwa likizo, huko nyumbani nani alikuwa akiwaangalia? Akipatia mimba nyumbani utanibana mimi tena au utaibana shule? Nenda hospitali walipopima uliza utaambiwa, mimi siwezi kusema kitu.

“Hatuwezi kufundisha wajawazito, sisi ni shule yenye nidhamu kubwa sana, kuna watu wanatuchafua tu, hali ya elimu ilikuwa mbaya, lakini tumejitahidi kupunguza ziro kwa kiasi kikubwa.

“Mwaka 2017 kidato cha nne kulikuwa kuna ziro 69, mwaka  2018 kulikuwa kuna ziro 67 ila mwaka jana tuna ziro 19 tu, tumejitahidi na tunaendelea kujitahidi,” alisema Mfaume.

Kuhusu shule kuwa katikati ya Jiji na kukosa uzio, alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli (TRL), Masanja Kadogosa aliahidi kujenga uzio wakati wa mahafali ya Novemba mwaka jana na Jumamosi ya wiki iliyopita alifika kutimiza ahadi yake.

Alisema sababu ya kuahidi ni kutokana na kusoma katika shule hiyo hivyo kuamua kurudisha shukrani.

“Ameishakuja na hivi karibuni itaanza kujengwa, lakini pia wazazi na walezi kuna kiasi cha fedha wamechanga, tutajenga uzio kama maagizo ya Jafo (Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo) aliyoyatoa kwetu,” alisema Mfaume.

Kuhusu wanafunzi kuzagaa mitaani wakati wa masomo, alisema jambo hilo si la kweli na kwamba wanafunzi huwa wanatoka kwa ruhusa maalumu.

“Ni wivu tu, unaona hiki kifaa, hapa mwanafuzi anabonyeza ndio anatoka kwenda mfano kanisani au msikitini, sisi hatufanyi kazi kwa kubahatisha, tunaijua kazi yetu na mimi nashangaa kauli hizi zinatoka wapi,” alisema Mfaume.

Pia, alisema wameendelea kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita kutokana na walimu kujitoa pamoja na kusimamia nidhamu.

“Kama huna nidhamu huwezi kusoma kwetu, sisi ni wafuasi wa nidhamu, ndiyo maana matokeo yetu ya kidato cha sita yanakuwa mazuri, hao wanaozusha huo uzushi, wanaohusika wawachukulie hatua kali za kisheria,” alisema Mfaume.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles