Rais Donald Trump wa Marekani ameamuru kufanyika mabadiliko ya uongozi katika Wizara ya Usalama wa Ndani.
Ikulu ya Marekani imesema kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya upelelezi wa jinai na ulinzi wa viongozi wa Serikali Randolph Tex Alles amejiuzulu na nafasi yake itajazwa mwezi Mei na afisa mwingine wa upelelezi James Murray.
Mabadiliko hayo ni ya pili katika Wizara ya Usalama wa Ndani katika siku mbili tu. Jumapili iliyopita, Kirstjen Nielsen aliachia wadhifa wake kama Waziri wa Usalama wa Ndani.
Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai yuko chini ya Waziri wa Usalama wa Ndani na ana jukumu la kumlinda rais na viongozi wa mataifa wanaozuru Marekani. Hakuna sababu yoyote rasmi iliyotolewa kuhusu kuondoka kwa Alles.