NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mkuu wa Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI), Thomas Mayagilo, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh milioni 15 baada ya kupatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka na kughushi nyaraka.
Mayagilo, alifunguliwa mashtaka hayo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mbele ya Hakimu Mkazi, Catherine Kiyoja, katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Takukuru katika kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2013 iliwakilishwa na mawakili wawili ambao ni Veronica Chimwanda na Lupiana Mwakitobe.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Kiyoja alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne waliothibitisha tuhuma hizo.
Alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kwamba amewatia hatiani washtakiwa hao.
Alisema, Mayagilo ametiwa hatiani kwa makosa manne ambapo mashtaka matatu ni ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha sheria huku shtaka la nne likiwa ni kutumia nyaraka kudanganya majina ya waajiriwa ndani ya ofisi yake kinyume cha sheria.
“Mtuhumiwa kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa, mahakama imekukuta na hatia ya mashtaka manne ambayo ni matumizi mabaya ya madaraka na lile la kutumia nyaraka kudanganya majina ya waajiriwa.
“Hivyo shtaka la kwanza mpaka la tatu kila moja utalipa faini ya Sh milioni tano au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na katika shtaka la nne utalipa faini ya Sh milioni 15 au kwenda jela miaka mitano ili liwe funzo kwa wote wanaotumia vibaya madaraka yao,” alisema Hakimu Kiyoja.
Hata hivyo, Mayagilo aliachiwa huru baada ya kulipa faini hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, ilidaiwa kuwa kati ya mwaka 2007 na 2008 akiwa Mkuu wa Chuo cha DMI, aliajiri vijana wawili katika nafasi za Tutorial Assistance Marine na Tutorial Marine Transports bila kufanyiwa usaili.
Ilielezwa kuwa mara baada ya kuwaajiri vijana hao alitumia fedha za ofisi kuwalipa mishahara kinyume na utaratibu.
Katika shtaka jingine, Mayagilo alitumia nyaraka zisizo halali kudanganya kuwa waajiriwa hao walikuwa wamefanya usaili jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 6 kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2002.
Mayagilo alidaiwa kukiuka utaratibu kufuatia kushindwa kumuajiri kijana aliyeitwa kwa ajili ya usaili na kufaulu katika nafasi ya uhasibu lakini hakupewa ajira.