25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mkutano wa Trump, Kim wakatishwa ghafla

HANOI, VIETNAM

MKUTANO wa kilele baina ya Rais wa Marekani, Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ulikatishwa ghafla jana baada ya wawili hao kutoafikiana.

Akizungumza na wanahabari mjini hapa jana akiwa peke yake, Trump alisema alilazimika kuondoka mkutanoni baada ya Kim kutoa masharti yasiyowezekana.

Kim alitaka nchi yake iondolewe vikwazo vyote ilivyowekewa kwa uchochezi wa Marekani, kitu ambacho Trump alisema hasingekiruhusu bila upande wa Korea kukubali masharti kadhaa.

Hata hivyo Trump alisisitiza bado wana uhusiano mzuri na Kim na ana matumaini kwa siku za usoni.

Awali wakati wa hafla ya chakula juzi jioni ambako walimwagiana sifa, Trump na Kim walikuwa wameonesha matumaini ya kuimarisha uhusiano na kupiga hatua katika mazungumzo yanayolenga kuifanya Korea Kaskazini iachane na mpango wake wa nyuklia.

Huo ni mkutano wa pili wa kilele kati ya viongozi hao wawili baada ya kukutana miezi minane iliyopita nchini Singapore.

Trump na Kim waliondoka kutoka eneo la mkutano bila ya kutia saini taarifa ya pamoja wala kuhudhuria dhifa ya chakula cha mchana kilichokuwa kimepangwa baada ya mkutano huo na kurejea katika hoteli zao.

“Ilikuwa ni kuhusu vikwazo tu,” alisema Trump katika mkutano na wanahabari baada ya mkutano wake na Kim kuwa mfupi kuliko ilivyotarajiwa.

“Kimsingi walitaka vikwazo walivyowekewa viondolewe kiukamilifu, lakini hatuwezi kufanya hivyo bila makubaliano.

Marekani na Umoja wa Mataifa kwa pamoja waliiwekea vikwazo Korea Kaskazini baada ya taifa hilo kufanya mfululizo wa majaribio ya makombora ya nyuklia na makombora ya masafa marefu mwaka 2017.

Trump alisema Kim yu tayari kuharibu kituo cha utafiti wa nyuklia cha Yongbyon, iwapo Marekani itaondoa vikwazo, lakini hayuko tayari kuhusu maeneo mengine na silaha, hali iliyomlazimu kuvunja mazungumzo.

Awali baada ya hafla ya pamoja ya chakula cha jioni juzi, Ikulu ya Marekani ilisema viongozi hao wawili wanapanga kusaini “makubaliano ya pamoja” baada ya mazungumzo zaidi jana.

Hata hivyo, haikutoa maelezo yoyote kuhusu sherehe hiyo ya utiaji saini, ijapokuwa mazungumzo ya pande zote yamejumuisha uwezekano wa taarifa ya kisiasa ya kutangaza kumalizika kwa Vita ya Korea ya mwaka 1950 – 53, ambayo baadhi ya wakosoaji wanasema bado mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,211FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles