27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MKUTANO VYAMA VIKUU AFRIKA, CHINA ULETE MAPINDUZI

WIKI hii Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa vyama vya siasa barani Afrika na China ambao ulishikirisha  mataifa kadhaa ukiwa na lengo  moja la kujadili maendeleo.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, aliyewataka washiriki kujadili na kupata majibu ambayo yatafungua milango ya kulikomboa bara la Afrika.

Moja ya maelekezo ya Rais Magufuli, ni kutaka kuona vyama hivyo vinasaidia kwa kila namna kuwaletea wananchi maendeleo kupitia nyanja mbalimbali na fursa zilizopo katika nchi zao.

Tunakubaliana na Rais Magufuli kwamba kama vyama hivyo vitasimamia vizuri sera na miongozo vilivyojiwekea, hakuna shaka vitasaidia kuwaondoa wananchi wengi kwenye lindi la umasikini unaowakabili.

Tunasema hivyo kwa sababu bara la Afrika limebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, lakini zimekuwa haziwanufaishi wananchi zaidi ya kupelekwa nje ya nchi, hasa katika mataifa makubwa.

Mwenendo huo, umesababisha Afrika siku zote lionekana ni bara ombaomba licha ya utajiri mkubwa uliopo.

Tumefurahi kusikia maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na washiriki kukubaliana kuwa vyama vya siasa ni muhimu katika kujenga mataifa na uchumi imara, kwa kuhakikisha kunakuwa na usimamizi madhubuti wa rasilimali za nchi zao kwa manufaa ya watu wao.

Azimio jingine, washiriki hawa walikubalina kuwa ni kweli kuna makosa waliyoyafanya muda mrefu na kuvifanya vyama vya siasa katika Afrika kuwa ni mitambo ya kutafuta kura, badala ya kuwa nyenzo muhimu ya kujenga maarifa na fikra za kimapinduzi.

Tunatambua katika kufikia maendeleo makubwa hakuna njia ya mkato, ndiyo maana nchi kama China imeweza kusimama kwa sababu ya kusimamia misingi na sera zinazowekwa.

China ya leo si ile ya miaka ya nyuma, ambayo ilikuwa ombaomba. Sera madhubuti na vyama vya siasa vilivyopewa dhamana vimeweza kutanguliza masilahi ya wengi kuliko kundi  la watu wachache.

Pamoja na kuwa na sera za kikoministi, China imeweza kusimamia misingi ya maendeleo na haki za watu, ndiyo maana leo hii imeweza kupunguza umasikini kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wao.

Kutokana na hali hiyo, umefika muda wa viongozi wa Afrika kubadilika na kuachana na dhana ya kwamba wanafanya jambo fulani kwa manufaa ya vyao, maana tabia hii imeota mizizi katika mataifa mengi ya bara hili.

Kumekuwapo na tabia ya baadhi ya watawala wanapoingia madarakani, wanatanguliza masilahi yao, badala ya kuwatumikia wananchi.

Mkutano huo uwafungue macho na waonyeshe dhamira ya kufikia malengo waliyojiwekea.

Kwa mfano kama China wameweza, Tanzania tunashindwa nini kutokana na utitiri wa rasilimali zilizopo.

Ili tuyafikie maendeleo ya kweli, kwanza lazima vita dhidi ya rushwa iwe endelevu, mipango inayopangwa itekelezwe kwa wakati, bajeti zinazotengwa kwenda katika wizara mbalimbali, zipelekwe kama zilivyopitishwa bungeni.

Sisi MTANZANIA, tunasema China imeweza, kwanini Tanzania tushindwe? Jambo kubwa katika hili ni kujenga misingi ya nidhamu ndani ya vyama, na Serikali kutowaonea haya wale wote wenye nia ya kukwamisha maendeleo.

Chama kilichopewa dhamana ya kuongoza kihakikishe kinaisukuma Serikali yake kuongeza ajira na kusimamia misingi ya kujenga uchumi wa jamii huru inayojitegemea, badala ya kutegemea misaada kutoka ng’ambo.

Tunasisitiza kuwa mkutano mkuu wa vyama vya siasa Afrika na China, ulete mapinduzi katika nyanja za uchumi ili kuachana na utegemezi ambao umedumu miaka mingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles