Mkutano Mkuu Yanga Agosti 6 mwaka huu

Baraka DeusdeditNa WINFRIDA NGONYANI – DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeitisha Mkutano Mkuu wa wanachama utakaofanyika Agosti 6 mwaka huu, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya watani wao wa jadi, Simba kufanya mkutano wao mkuu na kupitisha mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kutoka kwenye mfumo wa wanachama hadi mfumo wa hisa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, iliwataka wanachama wa klabu hiyo kufika katika ukumbi huo mapema kwa ajili ya mkutano huo unaotarajiwa kuanza saa tatu kamili asubuhi.

Licha ya taarifa hiyo kutokutaja ajenda za mkutano, lakini MTANZANIA linafahamu kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwa na ajenda tano ambazo ni ripoti ya mkutano uliopita, maendeleo ya klabu, udhamini wa Quality Group, uwanja na mengineyo.

Mkutano huo unakuja miezi miwili baada ya klabu hiyo kufanya Uchaguzi Mkuu, Juni 11, mwaka huu katika ukumbi huo huo wa Diamond Jubilee na kuuweka uongozi mpya madarakani.

Katika hatua nyingine, Yanga SC itakuwa na mchezo wa kirafiki Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, ikiwa ni maandalizi ya mchezo wao wa Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika wiki ijayo dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here