Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mkutano wa pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Angola unaoendelea Zanzibar, unajadili mambo mbalimbali ikiwamo uchumi wa buluu.
Mkutano huo unaofanyika katika ngazi mbili za maafisa waandamizi na mawaziri ulianza Januari 14, 2024.
Lengo ni kujadili mambo muhimu ya ushirikiano ya siasa, diplomasia, ulinzi, usalama, Sheria, kilimo, uchumi wa buluu, biashara na uwekezaji.
Maeneo mengine ni pamoja na maendeleo ya miundombinu, ujenzi, uchukuzi, nishati, madini, tehama na huduma za kijamii za afya, elimu, sayansi, na teknolojia ya Habari na mawasiliano.
Mkutano huo pia unalenga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano ili kuchagiza maendeleo kati ya Tanzania na Angola.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa, amebainisha kuwa mkutano huo utatoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo uchumi.
“Katika mkutano wetu tunategemea kujadili masuala ya uchumi hususan msingi wa diplomasia ya uchumi. Mkutano huu utatoa mipango na mikakati ya pamoja itakayoimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili,” amesema Balozi Mussa.
Balozi Said ameongeza kuwa mkutano huo unajenga na kuendeleza misingi madhubuti ya mashirikiano katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Angola unaendelea kuimarika zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias, amesema mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano imekuwa ikitoa fursa mbalimbali za kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya kipaumbele kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano itaendelea kujadili masuala ya kisekta katika maeneo mahususi ya ushirikiano katika nyanja za diplomasia, usalama, ulinzi na uboreshaji wa huduma za kijamii,” amesema Balozi Sardinha Dias.
Mkutano wa kwanza ulifanyika Oktoba, 1988 Jijini Dar es Salaam, kufanyika kwa mkutano huu wa piili kunafuatia kusainiwa kwa Hati mbili za Makubaliano (MoUs) za kuhuisha/kufufua Tu JPC na Hati ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola Februari, 2023 Addis Ababa.