28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Mkurugenzi wa Intelijensia ya Jinai wa Polisi atua Arusha kuchunguza mauaji ya wanawake

Janeth Mushi – Arusha

MKURUGENZI wa Intelijensia ya Jinai wa Jeshi la Polisi nchini, Charles Mkumbo, amewataka wananchi wa Arusha kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kukomesha matukio ya kikatili dhidi ya wanawake yaliyojitokeza hivi karibuni katika Kata ya Olasiti.

Hivi karibuni kumeibuka vitendo vya ukatili ambapo baadhi ya wanawake wanabakwa na kuuwawa katika eneo hilo ambapo hadi sasa chanzo cha matukio hayo hakijajulikana.

Mkumbo aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara ulifanyika Kata ya Olasiti ambapo pia ulishirikisha wananchi wa Kata ya Muriet.

Lengo la mkutano huo ulikuwa ni kuweka mikakati ya pamoja katika kukomesha matukio hayo ya kikatili.

Alisema jeshi hilo limejipanga kumaliza vitendo hivyo ikiwemo kuimarisha ulinzi na kutaka jamii kutoa taarifa za kuwafichua wahalifu na watahakikisha wananchi wanafanya shughuli zao katika hali ya usalama zaidi.

“Tumekutana hapa kubaini chanzo cha tatizo na tujadiliane kwa pamoja nini kifanyike na ndiyo maana tunatoa wito mtoe taarifa na kuwafichua wahalifu kwani tunaishi nao kwenye jamii zetu ,tunategemea ushirikiano wenu zaidi.

“Suala la ulinzi na usalama ni la kila mmoja wetu siyo polisi pekee.Tumejipanga vyema kuhakikisha mnaendelea kufanya shughuli zenu katika hali ya amani, hivyo kuna haja ya kuboresha zaidi ulinzi shirikishi kuanzia ngazi za mtaa,”alisema.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Alex Martin, alilishukuru jeshi hilo kwa jitihada za haraka walizozichukua mara baada ya kutokea kwa matukio hayo ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria.

Aliomba jeshi hilo kusaidia ujenzi wa kituo kidogo cha polisi katika kata hiyo na kuipa Kata ya Muriet na Olasiti hadhi ya wilaya ya kipolisi ili kusaidia kumaliza matukio hayo ya kikatili dhidi ya wanawake na vitendo vya kihalifu kwa ujumla.

Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Oliver Mbowe, alisema ni wakati wa wazazi na walezi kukumbuka wajibu wao malezi bora kwa watoto ili kutokomeza kizazi kisichokuwa na maadili mema.

Awali mwishoni mwa mwaka jana Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani hapa, Jonathan Shanna, alisema wanashikilia watu nane wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo huku baadhi yao wakidaiwa kukutwa na vielelezo ikiwemo simu za mikononi za marehemu.

Wakati jeshi hilo likishikilia watuhumiwa hao, baadhi ya wananchi wa kata hiyo, wameendelea kutoa kilio chao kwa Serikali kutokana na hofu ya usalama wao inayosababishwa na kukithiri kwa matukio hayo katika eneo hilo.

Kwa upande wa baadhi ya wanawake waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutokutajwa majina yao kwa kuhofia usalama wao, walidai matukio hayo yanahusishwa na imani za kishirikina.

Wakati wakidai hayo wengine walidai ulevi na matumizi ya dawa za kulevya kwa baadhi ya vijana ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia kukithiri kwa matukio hayo.

 Hilo ni eneo la pili kukumbwa na matukio hayo ya kikatili mkoa wa Arusha ambapo baada ya  Mto wa Mbu wilayani Monduli, ambapo kuanzia mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu kuliibuka matukio hayo ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina na kukamata wahusika wa vitendo hivyo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles