22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi Usalama wa Taifa astaafu

Rashid Othman
Rashid Othman

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rashid Othman, amestaafu rasmi.

Othman, aliteuliwa kushika wadhifa huo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Agosti 20, 2006,  akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mtangulizi wake Apson Mwang’onda aliyestaafu Agosti 21, mwaka 2006 kwa mujibu wa sheria.

Kigogo huyo wa Usalama wa Taifa, aliyeapishwa kushika nafasi hiyo Agosti 21, 2006 amehudumu katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka 10.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa, Othman alistaafu Agosti 19, mwaka huu na nafasi yake kwa sasa inakaimiwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, George Madafa.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa Othman, anatajwa kuwa ni mtu aliyefanikiwa kuimarisha ulinzi pamoja na kuwa na maofisa wenye kuzingatia maadili ya kazi.

“Tunajua kuna wakati Idara iliyumba kidogo lakini kwa kipindi cha Othman tutamkumba kwa mambo mengi ikiwemo kurudisha nidhamu kwa maofisa nchi nzima. Ilifika wakati wengine walikuwa hawana maadili ya kazi lakini kwa sasa tunajivunia Othman na kwa hakika anakwenda kupumzika lakini tutamkumbuka,” kilisema chanzo chetu.

Waliowahi kuongoza usalama

Kwa miaka kadhaa Idara hiyo iliongozwa na vigogo kadhaa waliobobea katika masuala la Ulinzi na Usalama wakiwamo; Emir Mzena, Lawrance Gama,  Hans Kitine ambapo alipoondoka nafasi hiyo ilikamatwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga.

Mbali na hao nafasi hiyo ilishikiliwa pia na Amrani Kombe, Apson Mwang’onda, Rashid Othman huku mrithi wa nafasi yake akisubiri majaliwa ya Rais Dk. Magufuli, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi wa nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria.

Hii ndiyo Usalama

Katika mchakato wa mageuzi ambayo yamefanyika kwenye Katiba ya mwaka 1977, mfumo wa sheria na siasa za nchi, taasisi za dola zimejikuta zikiwa nyuma wakati vuguvugu la mageuzi likienda mbele.

Moja ya tasisisi zilizokumbwa na fukuto hilo ni Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambayo hapo awali chini ya utawala wa Serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, ilikuwa ni taasisi ambayo haikutambulika kisheria kutokana na muundo wake kuwa wa siri na wa gizani.

Matokeo ya utendaji wa idara hiyo uliiletea sifa ya kuogopwa na kuonekana ni chombo cha majungu, chuki na wauaji wa wananchi wenye misimamo tofauti na watawala serikalini.

Maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiwa katika muundo wa kiraia ni wanajeshi na idara hiyo ni chombo nyeti katika uhai wa dola..

Chombo hicho hufanya kazi kwa taratibu za idara zote za usalama wa taifa na huwa hakiingiliwa na mtu yeyote kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa hapa nchini mageuzi ya mwaka 1992 yaliyoanzisha mfumo wa vyama vingi na mabadiliko mengine ya kisheria na Katiba, yalisababisha kuundwa kisheria kwa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kutambulika rasmi kisheria hapa nchini kulianza mwaka 1996, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria ya Usalama wa Taifa Na.5 ya mwaka 1996 na kutambulika rasmi kwa jina la Tanzania Intelligence and Security Services (TISS).

Pamoja na hali hiyo imenyang’anywa mamlaka ya kukamata wahalifu ingawa wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere idara hiyo ilikuwa na mamlaka hayo chini ya ‘Detention Order’ yaani sheria ya kumuweka mtu kizuizini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles