25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MKURUGENZI TGT MBARONI KWA KUGUSHI NYARAKA


Na ABRAHAM GWANDU-ARUSHA

RAIA tisa wa kigeni akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Utalii ya Tanzania Game Tracker (TGT)  iliyopo eneo la Ngaramtoni ya chini wilaya ya Arumeru Mkoani, Michel Allard wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kughushi nyaraka mbalimbali za serikali kinyume cha sheria.

Mkurugenzi huyo raia wa Ufaransa  kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa idara ya uhamiaji Mkoa wa Arusha  wanatuhumiwa kushirikiana kula njama na kufanikiwa  kughushi vibali vya kuishi nchini na kufanya kazi .

Wengine walioshikiliwa na kuhojiwa na polisi na nchi wanazotoka  ni pamoja na Hendrikus Van der Goot (Uholanzi), Cliff  Durell Hunter(Afrika Kusini), Nana Grosse Woodley (Ujermani), Nicolas Carel Stubbs (Afrika Kusini) na Andrea Theresa Hartmann(Ujermani).

Raia wengine waliogushi nyaraka hizo za kuishi na kufanya kazi nchini toka mwaka 2015 na jambo lililosababisha serikali kukosa mapato ni pamoja na Priya Shah (Uingereza),Wesley Khamasi Guyavi (Mkenya) na Chinnadurai Vellaichamy (India).

Akizungumza na waandishi jana mjini hapa Ofisa Kiongozi wa Idara ya Kazi Mkoa wa Arusha, Yusuph Nzugille alithibitisha kukamatwa kwa raia hao kutokana na kupata taarifa ambazo walizifanyia kazi kwa kufanya ukaguzi wa kustukiza kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola .

Alisema walilazimika kuchukua hatua hiyo kwa mujibu wa sheria mpya ya kuratibu ajira za wageni nchini ya  mwaka 2015  ambayo inatamka wazi kuwa vibali vyote vya kufanya kazi vinatolewa na kamishna wa kazi katika Wizara ya kazi na idara ya uhamiaji imebakiwa na jukumu la kutoa vibali vya ukaazi (resident permit ).

“Nianze kwa kusema hivi, ni  kweli tumekamata raia hao wakifanya kazi TGT wakiwa na vibali vya kugushi vya kufanya kazi lakini hata vile vya kuishi nchini tunamashaka navyo isipokuwa wenye kusema ni halali au la ni uhamiaji,” alisema Nzugille.

Wakili wa raia hao wa kigeni, Wilfred Mawalla alisema wateja wake hawana makosa yoyote kwani waliamini nyaraka hizo ni halisi kwa sababu aliyewaandalia ni afisa wa idara ya serikali.

“Wateja wangu mpaka sasa hawana makosa, waliamini nyara wanazotuhumiwa nazo kuwa ni halisi ndio maana walijiamini kuishi na kufanya kazi nchini, hizi tuhuma za kugushi zielekezwe kwa maofisa wa idara za serikali waliohusika,” alisema Wilfred.

Akizungumzia tukio hilo,Naibu Kamishina wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Vitalis Mllayi  alikiri kuwa ofisi yake inalijua suala hilo ambapo alisema kwa sasa hawana mamlaka kwani lipo chini ya kikosi kazi maalumu ambacho kinatoka makao makuu ya Uhamiaji jijini Dar es salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles