24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi OBC aandika barua kwa DPP kukiri uhujumu uchumi

Janeth Mushi -Arusha

MKURUGENZI wa Kampuni ya Otterlo Business Limited (OBC) kutoka Falme za Kiarabu, Isaya Mollel, amemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kukiri mashtaka yake yakiwemo ya utakatishaji fedha, kukwepa kodi na kusababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 2.8.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 22 ya mwaka huu, OBC na Mollel wanakabiliwa na mashtaka hayo.

Jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Naomi Mollel na utetezi ukiwakilishwa na mawakili Daud Haraka na Goodluck Peter.

Jana kesi hiyo ilipangwa kutajwa mbele ya Hakimu Gwantwa Mwankuga, na Wakili Haraka aliieleza mahakama kuwa mteja wake ameandika barua kwa DPP kuomba kukiri makosa yanayomkabili.

“Mheshimiwa, mteja wetu ameandika barua kwa DPP ya kuomba kukiri, hivyo tunaomba tarehe ya karibu ili tuendelee na hatua zinazofuata,” alidai.

Awali Wakili Naomi aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuipangia tarehe nyingine kwani Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Niku Mwakatobe pamoja na Wakili wa Serikali, Martenus Marandu hawapo mahakamani.

Hakimu Mwankuga alikubaliana na hoja za pande zote na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21.

Mollel alifikishwa mahakamani mwanzoni mwa mwaka huu na kusomewa mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekomya.

Wakili huyo alidai shtaka la kwanza linalomkabili Mollel ni kughushi akidaiwa kati ya Septemba 15 mwaka juzi na Aprili 7 mwaka jana katika eneo lisilojulikana jijini Arusha, kwa nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka ambayo ni ankara ya malipo yenye namba 9091 ya Septemba 15, 2017.

 Alidai ankara (invoice) hiyo ilionyesha Kampuni ya OBC imeagiza gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa na chassis namba WDB62433615367735 kutoka Kampuni ya Everest Motors (FZD) ya Dubai, yenye thamani ya dola za Marekani 12,800 huku akijua ni uongo.

Shtaka la pili ni la kughushi linalomkabili mshtakiwa Mollel, anayedaiwa kutenda kinyume cha vifungu vya 333,335 (a) na 337 vya kanuni ya adhabu kama ilivyorejewa mwaka 2002. 

Katika shtaka hilo, Mollel anadaiwa kati ya Septemba 15 na Aprili 2, 2018 ndani ya Jiji la Arusha kwa nia ya kudanganya, alighushi ‘invoice’ iliyokuwa na namba 9092 ikionyesha OBC iliagiza gari aina ya Man Truck kutoka Kampuni ya FZD yenye thamani ya dola za Marekani 12,000.

 Wakili Tibabyekomya alitaja shitaka la tatu linalomkabili Mollel kuwa ni kutoa taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 203 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.

 “Machi 7, 2018 katika ofisi za forodha Holili mkoani Kilimanjaro, akiwa mkurugenzi wa kampuni, alisababisha kutolewa kwa maelezo ya uongo TRA kuwa kampuni imeingiza magari matatu aina ya Man Truck, Mercedes Benz mbili,” alidai Tibabyekomya.

 Alidai shitaka la nne linalomkabili Mollel na OBC ni kukwepa kodi kinyume na kifungu cha 203 (e) (iii) cha Sheria ya Usimamizi Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2014, kosa wanalodaiwa kulitenda kati ya Julai 2011 hadi Julai 2015 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Tibabyekomya alidai mahakamani hapo kuwa Mollel akiwa mkurugenzi na kampuni hiyo yenye leseni ya uwindaji wa kitalii, walikwepa kodi kwa kutoa maelezo ya uongo TRA kuonyesha kampuni hiyo imeagiza magari 31 na kukwepa kodi ya Sh bilioni 2.25.

 Kosa la tano lilalomkabili Mollel ni kukwepa kodi, ambapo anadaiwa kati ya Mei 25, 2013 na Februari 4,2015 katika Jiji la Dar es Salaam akiwa mlipakodi mwenye TIN namba 10183307 na akiwa na nia ya kukwepa kodi, alitengeneza nyaraka za uongo kwa TRA kuwa amelipia kodi ya magari sita. 

Tibabyekomya alitaja magari hayo kuwa ni Land Cruiser Pick Up tatu, Nissan Patrol tatu na kudai kutokana na udanganyifu huo amesababisha ukwepaji wa kodi Sh milioni 299.5.

Alidai shtaka la sita linalomkabili Mollel ni kukwepa kodi kinyume na kifungu cha 84 (1) (d) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, ambapo kati ya Julai 2016 na Februari 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam, akiwa na nia ya kudanganya TRA, alitengeneza nyaraka ya uongo iliyoonyesha amelipia kodi magari mawili aina ya Land Cruiser Pick Up na Ford Ranger na kukwepa kodi Sh milioni 111.3. 

Kosa la saba linalomkabili Mollel ni kukwepa kodi ambapo anadaiwa Februari 18 mwaka 2017 akiwa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kukwepa kulipa kodi, alitengeneza nyaraka ya uongo TRA na kuonyesha amelipia magari mawili aina ya Mercedes Benz na Nissan Patrol na kukwepa kodi Sh milioni 199.3.

 Wakili huyo alidai shtaka la nane ambalo ni utakatishaji fedha haramu linamkabili Mollel, analodaiwa kutenda kinyume na kifungu cha 12 na 13(1) (a) cha Sheria ya Utakatishaji fedha haramu  ya mwaka 2006. 

Wakili huyo alidai Aprili 3 mwaka jana katika  ofisi za forodha Holili, Kilimanjaro kwa ajili ya kuficha umiliki wa gari aina ya Man Truck lenye namba T 141 DNM, alificha umiliki wa mali hiyo kwa kusajili jina la OBC, akijua mali imetokana na kosa la utakatishaji fedha haramu (kughushi).

 Shtaka la tisa ambalo ni dhidi ya Mollel ni utakatishaji fedha haramu ambapo anadaiwa Aprili 3 mwaka jana akiwa ofisi za forodha Holili, alificha umiliki wa mali gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa na namba T 150 DNM, kwa kusajili mali kwa jina la OBC huku akijua mali imetokana na kosa la kughushi. 

Shtaka la 10 linalomkabili Mollel pamoja na OBC ni kusababisha hasara, ambapo kwa pamoja wanadaiwa kati ya Januari 2010 hadi Machi 2018 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwa nia ovu, walitengeneza nyaraka ya uongo kwa TRA na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 2.8.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles