27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mkurugenzi Jiji la Mwanza aonya wanasiasa

Hassana Hidda
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hassana Hidda

Na John Maduhu, Mwanza

MKURUGENZI Jiji la Mwanza, Hassana Hidda, amewataka wanasiasa kuacha siasa katika utekelezaji wa majukumu ya halmashauri hiyo, badala yake wasimamie sheria, taratibu na kanuni.

Mkurugenzi huyo ametoa msimamo huo baada ya kudaiwa baadhi ya wanasiasa kupinga uamuzi wa Baraza la Madiwani lililotaka kusafishwa Jiji kwa kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo katika maeneo yasiyoruhusiwa.

“Wanasiasa wana sehemu yao ya kutekeleza majukumu yao ya kisiasa, nasi kama wataalamu tunapaswa kuachwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, zoezi la kuwaondoa wamachinga liko kisheria na tutaendelea kuwaondoa,” alisema Mkurugenzi huyo.

Hidda alisema hakuna siasa katika kazi ya kuwaondoa wamachinga na kuwataka wanasiasa wanaowapotosha wafanyabiashara kuacha mara moja.

Mkurugenzi huyo alisema barabara iliyopo eneo la Makoroboi ambalo wamachinga wameondolewa linatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami hivi karibuni, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya Jiji la Mwanza kuweka lami katika barabara zote zilizopo katikati ya Jiji.

“Hali ya Jiji la Mwanza kwa sasa ni shwari, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaondoa wamachinga katikati ya jiji, kinachofanyika sasa ni kuweka mikakati ya kuwaondoa waendesha pikipiki na kuwazuia kuingia katikati ya jiji, hawa wataondoka baada ya kukamilika kwa utafiti wa vituo watakavyokuwa nje ya maeneo ya katikati ya jiji,” alisema Mkurugenzi huyo wa Jiji.

Akizungumzia kazi ya upimaji na ugawaji viwanja vilivyopo eneo la Luchelele, Kata ya Mkolani, Mkurugenzi huyo alisema kazi ya kulipa fidia wananchi ambao ardhi yao imechukuliwa inatarajia kuanza hivi karibuni.

“Kila kitu kiko tayari, tunasubiri Serikali ikamilishe taratibu fulani fulani na kisha tupewe mkopo na benki, tuna hakika ndani ya muda mchache zoezi la kulipa fidia na kuuza viwanja vya Luchelele litakuwa limeanza,” alisema Hidda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles