26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MKURUGENZI JAMII FORUMS: UHURU WA HABARI KITANZINI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


 

JAMII FORUMSMKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited inayoendesha mtandao wa Jamii Forums, Mexence Melo, ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya kutimiza masharti ya dhamana, huku akisema kuwa kukamatwa kwake ni ishara mbaya kwa vyombo vya habari.

Melo alitimiza masharti ya dhamana jana baada ya kushindwa kufanya hivyo mwishoni mwa wiki na kusababisha kwenda gerezani.

Akizungumza nje ya mahakama, Melo alidai kukamatwa kwake ni ishara mbaya kwa vyombo vya habari, kwani ni shambulizi kwa uhuru wa vyombo vya habari na imekuwa mara ya kwanza mtu kuwekwa ndani kwa kulinda uhuru wa kuongea.

“Nawahakikishia watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums kwamba upo salama na hakuna taarifa zozote zilizochukuliwa wala zitakazochukuliwa na mtu yeyote.

“Sina maana ya kuipinga Serikali, isipokuwa tunapinga sheria dhalimu ya ukandamizaji ambayo tukiendelea kuiachia itatuangamiza wote,” alisema.

Alisema anashukuru jamii ya mitandao na vyombo vya habari kwa kuibua mijadala iliyoishinikiza Serikali imwachie kwa dhamana.

“Kufikishwa kwangu mahakamani inatokana na msimamo wangu wa kulinda siri za watumiaji wa mtandao wa Jamii Forum ambao polisi walitaka kuudukua.

“Mimi kufikishwa mahakamani ni mfano tu, kwani msishangae mkaona wengine wanafikishwa, lakini hatupaswi kuhofia wala kuogopa, kikubwa ni kulinda siri za watumiaji wa mitandao,” alisema.

Melo aliwataka waandishi wa habari kupambania uhuru wa kujieleza aliodai kuwa upo kwenye hatari kubwa ya kuangamizwa, kutokana na sheria mpya ya mitandao kuwa kandamizi.

Melo anakabiliwa na kesi tatu kwa mahakimu watatu tofauti. Kesi namba 457 iliyokuwa kwa Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa ndiyo aliyoshindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Katika kesi hiyo, Wakili wa Jamhuri Salum Mohammed alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kwamba kati ya Aprili mosi na Desemba 13, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa kampuni ya Jamii Media Limited inayoendesha mtandao maarufu wa Jamii Forums, alishindwa kutoa taarifa za kiuchunguzi za makosa ya mtandao kwa maofisa wa Jeshi la Polisi nchini kupitia mtandao wake.

Katika maelezo ya kosa hilo, Wakili Salum alidai kwamba tukio hilo lilitokea kati ya Mei 10 na Desemba 13, mwaka huu katika ofisi za Jamii Forums zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam.

Inadaiwa mshtakiwa akiwa anafahamu kuwa Jeshi la Polisi linafanya upelelezi wa makosa ya mitandao mbalimbali ya kijamii, kwa makusudi alizuia uchunguzi katika ofisi yake.

Mshtakiwa alikana kutenda makosa yanayomkabili na upelelezi unaendelea.

Alipewa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja na hatakiwa kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali.

Pia anakabiliwa na kesi nyingine namba 458 ambayo alipandishwa tena kizimbani na kusomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.

Wakili wa Serikali, Salum alidai kwamba mtuhumiwa anakabiliwa na kosa la kumiliki na kutoa huduma katika mtandao wa kijamii bila kuwa na kibali kitu ambacho ni kinyume cha sheria na taratibu za mitandao nchini.

Salum alidai kuwa kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, mwaka huu huko Mikocheni akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, alikuwa anamiliki mtandao huo kinyume cha sheria kwa sababu hakusajili katika tovuti ya Tanzania.tz.

Katika shtaka la pili katika kesi hiyo, Melo, anadaiwa kati ya Januari 26 na Desemba 13, mwaka huu huko Mikocheni akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alishindwa kutoa taarifa ili kukamilisha upelelezi wa Jeshi la Polisi.

Mshtakiwa alikuwa akiwakilishwa na Wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole.

Katika kesi nyingine mbili, mshtakiwa alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa, alitakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua na watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni 10 kwa kila mmoja.

Kesi hizo ziliahirishwa hadi Desemba 29, mwaka huu zitakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles