27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi akerwa na mauaji ya mifugo

ng'ombeNa Ruth Mnkeni, Dar es Salaam

WIZARA ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, imeonesha kukerwa na mauaji ya mifugo, huku ikiwaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa wizara hiyo, Dk. Abdu Hayghaimo alisema hali hiyo inasababisha madhara makubwa ikiwamo uvunjifu wa amani, vifo vya binadamu na mifugo.

Alisema si jambo la busara kuadhibu wanyama kwenye maeneo ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji, kwa sababu hawana hatia yoyote.

“Wananchi wenye tabia hii wanatakiwa kuacha mara moja, ukweli usiopingika migogoro hutokea baada ya wanyama kuongozwa na binadamu kwenye maeneo yasiyowahusu, ni kosa kubwa kuwaadhibu wanyama hasa ukizingatia kwamba wanyama hawana uamuzi zaidi ya kumtii mtu aliyewachunga.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Ustawi wa Wanyama ya mwaka 2008 sura ya 154 kifungu cha 4; wanyama wanayo haki ya kupewa chakula, maji, mahali pazuri pa kupumzika, kulindwa dhidi ya maumivu yoyote, magonjwa na mateso ikiwa ni pamoja na kuwasababishia kifo.

“Pia sheria hii katika vifungu vya 49 mpaka 58, inaainisha taratibu za kufuatwa pale ambapo mnyama amekutwa kwenye eneo lisiloruhusiwa.

“Vitendo vilivyofanywa kwa wanyama kwenye Kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero ni kosa kwa mujibu wa sheria,”alisema.

Hata hivyo, aliitaka jamii itafute suluhu ya migogoro hiyo kwa kupitia kamati zitakazosimamia matumizi endelevu ya ardhi kwa mujibu wa waraka unaoandaliwa na wizara yake.

Alisema wizara itahakikisha kamati hizo zinaundwa kwa ufanisi katika kuzingatia taratibu, kanuni na sheria husika na uwakilishi wa pande zote mbili wakulima na wafugaji.

Hivi karibuni ng’ombe 79 waliuawa  kutokana na mapigano kati ya wafugaji na wakulima  yaliyotokea katika Kata ya Kanga Kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles