Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo (DED), Mkoa wa Morogoro, Agnes Mkandya, jana aliangua kilio wakati akihojiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Tukio hilo la aina yake lilitokea mjini hapa katika Ukumbi wa Msekwa baada ya wajumbe wa kamati hiyo kumwuliza maswali juu ya ubadhirifu wa fedha katika halmashauri yake.
Kabla ya kumwaga machozi, mkurugenzi huyo aliulizwa maswali mbalimbali na kuyajibu, lakini Mbunge wa Viti Maalumu, Leah Komanya (CCM) alipouliza juu ya ubadhirifu wa fedha katika halmashauri yake, alianza kupoteza mwelekeo na kuanza kulia.
Katika swali lake, Komanya aliuliza ni kwa nini katika Halmashauri ya Gairo kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha unaofanywa na watendaji mbalimbali kwa kutumia karatasi maalumu.
“Ubadhirifu huo hauko kwenye mapato peke yake kwani pia watendaji wamekuwa wakiiba kwa kutumia ‘cabon slip’ na kuikosesha halmashauri mapato.
“Kwa hiyo, naomba kuuliza mmekuja na majibu gani juu ya masuala hayo?,” alihoji Komanya.
Akijibu swali hilo, Mkondya alikiri kuwapo kwa wizi huo kupitia cabon slip na kusema tayari wameshamkamata mtumishi mmoja ingawa wanaendelea kuwatafuta wengine.
“Kamati ielewe kwamba, Halmashauri ya Gairo imeoza na ni chafu kwa sababu kuna ubadhirifu mkubwa. Tayari nimewasimamisha kazi wakuu tisa wa idara, lakini kumbukeni na mimi ni mgeni sina muda mrefu.
“Lakini hivi sasa tunajiandaa kuanza kutumia mashine za EFD na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iko tayari kutuunganisha katika mfumo huo,” alisema Mkondya.
Baada ya kutoa maelezo hayo na kuvuta pumzi, alianza kulia na kuwafanya wajumbe wa kamati hiyo kuanza kumbebeleza.
Wakati wabunge wakimtuliza, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Vedastus Ngombale Mwiru, alimtaka aondoe woga kwani maswali aliyokuwa akiulizwa yalikuwa ya kawaida.
Hata hivyo, Ngombale alimtaka Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo ya Gairo ajibu maswali mengine kwa kuwa ana muda mrefu mahali hapo.
“Ni kweli, mkurugenzi ni mgeni, lakini hapa yupo mkaguzi wa ndani, hebu ajibu swali hilo la ubadhirifu wa fedha,” aliagiza Ngombale.
Katika maelezo yake, mkaguzi huyo wa ndani alisema tatizo lililopo katika halmashauri hiyo ni mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuwa hayakusanywi kwa njia ya kielektroniki.