26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Mkulo atinga mahakama ya mafisadi, atoa ushahidi

*Ni katika kesi ya kina Kitilya, mvutano waibuka

KULWA MZEE  -DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo  wa Serikali ya awamu ya nne, ameibua mvutano mahakamani wakati akielezea mikopo yenye masharti nafuu na kutaka kutoa kielelezo cha  barua iliyoambatanishwa na maelekezo ya kina kuhusu mapendekezo ya kutaka kuikopesha Serikali Dola za Marekani milioni 550

Mkulo alidai hayo jana katika  Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi wa kesi inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Harry Kitilya na wenzake.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hillah mbele ya Jaji Immaculata Banzi, shahidi huyo alidai barua hiyo ilitoa Benki ya Stanbic na Standard Charterd ya Uingereza ambapo yeye alitoa maelekezo katika hiyo barua.

“Kama Waziri wa Fedha majukumu yangu yalikuwa kuandaa bajeti ya Serikali na kusimamia matumizi na madeni. Vyanzo vya mapato ya Serikali ni kodi inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya miradi mikubwa ya Serikali kutoka kwenye taasisi za fedha za kimataifa kama Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani na taasisi zingine.

“Vyanzo vingine, ni misaada ya kimataifa, mikopo ya muda mfupi na Serikali inakopa, bajeti huwa haitoshelezi matakwa yote ya Serikali, baada ya kuandaa na kubaini kiasi kilichopungua tunatafuta mikopo yenye masharti nafuu,” alidai Mkulo.

Alidai benki zote zinazotoa mikopo ya biashara yenye riba kubwa, lakini pia kuna benki zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Serikali.

Wakili wa mshtakiwa wa kwanza, Dk. Masumbuko Lamwai alipinga shahidi kuzungumzia aina hizo za mikopo akidai shahidi anatakiwa azungumzie ushahidi uliopo katika maelezo yake aliyotoa na si vinginevyo.

Alidai kinachoelezwa ni kitu kipya hakipo kwenye maelezo yake ya ushahidi,  hivyo aliiomba mahakama iwaruhusu wawasilishe pingamizi kisheria.

Akijibu Wakili wa Serikali Mkuu, Osward Tibabyekomya alidai alichokuwa anafanya shahidi ni kutoa ufafanuzi kuhusiana na kazi anazofanya.

Kutokaja na hali hiyo, Jaji Banzi alitoa maelekezo kwa  upande wa Jamhuri, ujikite katika maelezo ya shahidi, shahidi atafafanua pale panapohitaji ufafanuzi.

Wakili Hillah, aliendelea kumuongoza shahidi kuelezea mikopo yenye masharti nafuu ambapo alieleza kuwa muda wa kurejesha mkopo .

“Nikiwa waziri, baada ya bajeti kupita na kubaini kiasi kilichopungua, waziri anapewa dhamana ya kukopa mikopo yenye masharti nafuu ili kufidia upungufu kwenye bajeti.

“Ili kupata mikopo hiyo Serikali inaweza ikaitisha mabenki kadhaa ili wapeleke mapendekezo  au benki zenyewe zinaweza kuwasilisha,”alidai.

Katika hilo la mapendekezo kuna taarifa muhimu, ikiwamo kiasi cha mkopo, muda, riba na vitu vingine.

Mkulo alidai baada ya kuwasilisha mapendekezo kwa Waziri wa Fedha, anasoma kisha anapeleka kwa wataalamu ambao ni idara ya sera ili waifanyie uchambuzi kama itakidhi mahitaji itapelekwa katika kamati ya wataalamu wa usimamizi wa madeni.

Kamati  ya Usimamizi wa Madeni, inaongozwa na Kamishna wa Sera na naibu wake ni msaidizi wa kamishna, wakishafanya uchambuzi mapendekezo wanapeleka kwa kamishna wa mikopo.

Nyaraka wanazopeleka ni uchambuzi wa mkopo, mchanganuo na maoni ya wajumbe wa kamati hiyo. Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa madeni kazi yao kuchambua mapendekezo na kuyapeleka kwa waziri ambaye akiridhia anatoa kibali cha Serikali kukopa.

“Mwaka 2008 hadi 2012, aliyekuwa Kamishna wa Fedha ni Bedason Shallanda, hadi nastaafu nilimuacha Bedason, aliyekuwa msaidizi wa kusimamia madeni ni Afred Misana.

“Mwaka 2010 hadi 2011, Serikali katika bajeti yake kulikuwa na upungufu ikakopa Dola za Marekani 250 kutoka Benki ya Stanbic, 2011, 2012 pia kulikuwa na upungufu wa Dola za Marekani milioni 800, Serikali ilichukua hatua ya kutafuta mkopo,” alidai Mkulo.

Alisema Serikali ilipata mapendekezo kutoka benki mbalimbali, Stanbic, City Benki Marekani, Barclays ya Uingereza, HSBC ya Uingereza, Exim benki na zingine.

Mapendekezo  ya Benki ya Stanbic yaliwasilishwa mwaka 2012 kwa Waziri wa Fedha ambaye aliisoma na kuagiza ipelekwe kwa Kamishna wa Sera kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi.

“Nilitoa maelekezo kwa maandishi, kwa barua iliyoambatanishwa na maelekezo ya kina kuhusu mapendekezo ya kutaka kuikopesha Serikali Dola za Marekani milioni 550,” alidai.

Shahidi aliomba kutoa barua hiyo kama kuelelezo lakini mawakili wa utetezi walipinga kupokelewa kwa sababu ina masharti ya kutotumika vinginevyo.

Akijibu Hillah alidai hoja hizo hazina msingi wowote kisheria na nyaraka zipokelewe takwa la masharti haliwezi kutumika  kuzuia.

Baada ya mabishano hayo, Jaji Banzi aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa uamuzi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2019, ni mshindi wa mashindano ya urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.

Wengine ni maofisa wawili wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda,  ambaye kwa sasa yuko  Ofisi ya Waziri Mkuu na  Alfred Misana, ambaye kwa sasa yuko  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwamo ya kuisababishia  Serikali hasara ya kiasi cha Dola milioni  sita, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles