Nathaniel Limu-Singida
JESHI la Polisi mkoani Singida,limeanzisha msako mkali wa kumsaka mkufunzi msaidizi wa jeshi la akiba (mgambo), Said Athumani Ng’imba mwenye namba MG129191 kwa tuhuma ya kutoa adhabu kwa wanafunzi wawili watumbukie kwenye dimbwi na kusababisha vifo vyao.
Wanafunzi waliofariki dunia,ni Emmanuel Hamisi (20) mkazi wa Kijiji cha Mudida na Ismael Hussein (22) mkazi wa Kijiji cha Sepuka.
Wanafunzi hao walikuwa wanahudhuria kozi ya mafunzo ya awali ya jeshi la akiba ambayo yanaendelea kufanyika Kijiji cha Mudida.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike alisema tukio hilo lilitokea Novemba 20, mwaka huu katika Kijiji cha Mudida.
Alisema wanafunzi walipewa adhabu hiyo, baada ya kutokuhudhuria vipindi vya mafunzo vya siku moja ya Novemba 19, mwaka huu.
Alisema kutokana na kukosa vipindi,mkufunzi Ng’imba aliwapa adhabu ya kutumbukia kwenye dimbwi lililokuwa limejaa maji.
“Jeshi la polisi likishirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, lilifanya juhudi kubwa kuwaokoa,liliwaopoa kutoka majini wakiwa tayari wamefariki dunia.
“Baada ya kutumbukia,walizama ndani ya dimbwi na hawakuonekana,kitendo hiki kilisababisha mkufunzi msaidizi kutimua kusikojulika hadi sasa.Tayari tumeanza kumsaka kwa nguvu na tunatarajia muda si mrefu atakuwa mikononi mwetu,”alisema.
Habari kutoka eneo la tukio,zinadai wanafunzi hao kabla ya kutumbukia,walibebeshwa kila mmoja mfuko mgogoni uliojazwa mchanga.
Wakati huo huo,Njewike alisema wamafanikiwa kumkamata Kitundu Ismail (29) mkazi wa Kijiji cha Mwau kwa tuhuma kuhifadhi dawa za kulevya aina ya bangi misokoto 419.Alikuwa ameificha chumbani kwake.
Alisema kwa sasa wanaendelea kumhoji ili kujua mtandao wa matumizi ya madawa hao,ili waweze kuudhibiti.