MKUDE, NYONI WATUNISHA MSULI SIMBA

0
1015

Mwandishi wetu -Dar es salaam

WACHEZAJI Jonas Mkude, Clatous Chama na Erasto Nyoni huenda wakaingia matatizoni na klabu yao ya Simba, baada ya kudaiwa kukaidi kusaini barua za wito wa kuhudhuria kikao kati yao ya uongozi, ili kujieleza kwanini walishindwa kuambatana na wenzao katika safari ya Kanda ya Ziwa.

Chama  na Mkude ambao wanacheza nafasi ya kiungo na Nyoni ambaye ni beki hawakuambatana na kikosi cha Simba Kanda ya Ziwa, kwa ajili ya michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United.

Wachezaji hao kila mmoja anadaiwa kutoa sababu tofauti zilizowakwamisha kusafiri na wenzao, ingawa uongozi wa klabu hiyo haujaridhishwa nazo hivyo unataka kukutana nao ili kupata maelezo ya kina kabla ya kuamua vinginevyo.

Licha ya uongozi wa Simba kutokuwa tayari kuweka wazi, lakini chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kililiambia MTANZANIA kuwa Mkude hakuweza kusafiri baada ya kuchelewa ndege siku ya safari, wakati Nyoni alidai kuuguliwa na mwanawe huku kilichomkwamishwa Chama hakikujulikana.

Simba iliikabili Kagera Septemba 26, Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na kushinda mabao 3-0 kabla ya Septemba 29 kuumana na Biashara na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. 

Jana wachezaji hao tegemeo ndani ya timu hiyo hawakushiriki mazoezi na wenzao kwenye Viwanja vya Gymkhana jijini hapa.

Gazeti hili lilipotaka kujua kutoka kwa Meneja wa timu hiyo Richard Rweyemamu kulikoni wachezaji hao kukosekana mazoezini,  licha ya kikosi hicho kurejea Dar es Salaam hakuwa tayari kulizungumzia.

Hata hivyo chanzo kingine kililiambia MTANZANIA  kuwa,  Mkude, Nyoni na Chama walipelekewa barua za wito na kutakiwa kuzisaini ili kuonyesha zimewafikia lakini kati yao hakuna aliyekuwa tayari kufanya hivyo.

“Wamepewa barua za wito wa kuitwa ili wahojiwe lakini wamekataa kuzisaini, inawezekana kuwa watu wanawadanganywa, wanafanya mambo ya kitoto kwa kweli.

“Kinachofuata hapa watajadiliwa na kamati ya nidhamu kabla ya kutoa uamuzi ni hatua gani wachukue wachukuliwe,”kilisema chanzo hicho.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza akiwa ameambata na timu hiyo Bukoba na kisha Mara alisema hatma ya Mkude na wenzake itajulikana baada ya kurejea Dar es Salaam.

Juhudi za kuwapata wachezaji hao ili wazungumze  kuhusiana na tuhuma za kukaidi kupokea barua za wito hazikufanikiwa baada ya simu zao kutopokelewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here