30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Mkotya atangaza rasmi kumvaa Nkamia

mkotya atangaza niaNA PENDO MANGALA, DODOMA
MHARIRI Msanifu wa gazeti la MTANZANIA, Hamisi Mkotya, ametangaza rasmi nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Chemba mkoani hapa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jimbo la Chemba linaongozwa na Mbunge Juma Nkamia ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mkotya alitangaza nia hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza vipaumbele vyake endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo.
“Kipaumbele changu cha kwanza endapo nitafanikiwa kuwa mbunge wa Chemba, nitahakikisha kunakuwa na maji kwani kero hii ni kubwa na imesababisha wakazi wa Chemba kuchangia maji ya kunywa na fisi.
“Inasikitisha katika karne hii, bado kuna wananchi katika Jimbo la Chemba wanachangia maji na fisi, unakuta mama anachota maji hapa na ng’ombe anakunywa maji pale, maji hayo yanakwenda kutumika katika matumizi ya kawaida ya binadamu,” alisema.
Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kukuza uchumi kwa kuinua kilimo katika kuwawezesha wakulima wa Chemba kulima kilimo bora kwa kutumia mbinu bora ikiwamo wataalamu wa ugani.
Mkotya alisema kutokana na uhaba wa vituo vya afya katika wilaya hiyo, wakazi wake hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya nje ya jimbo hilo.
Alisema akifanikiwa kutwaa nafasi hiyo, atahakikisha anacheza na vitu vitatu ambavyo ni ukweli, uwazi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anasimamia vizuri fedha za Mfuko wa Jimbo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa katika kuharakisha maendeleo.
“Nitajitoa kwa nguvu zangu kuisimamia Halmashauri ya Chemba kuhakikisha inatenga fedha kiasi cha asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya vijana na akinamama,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles