23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mkonge: Kutoka alama ya mpaka hadi zao kuu la biashara

SuzaneNA MAREGESI MAPUL, (OUT) DAR ES SALAAM

KATIKA miaka ya hivi karibuni zao la mkonge limekuwa linavutia uwekezaji wa vitega uchumi vya nchi mbalimbali duniani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyopo katika sehemu ya joto kutokana na hali ya hewa inayofaa kulima zao la katani kwa ajili ya kilimo biashara.

Kwa wastani, mkonge unaweza kuishi miaka 13 hadi 14, ambapo majani yake yanaweza kufikia 200 hadi 300 na yanaweza kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile kamba nene, magunia, heleni na mazuria.

Kadiri miaka inavyoenda zao hili linakuwa linaongeza thamani katika uzalishaji wa bidhaa zake kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia, linazalisha bidhaa mbalimbali katika mitambo, mawasiliano, usafiri baharini, mafuta, misitu na kilimo.

Hii ni kutokana na matumizi ya mkonge kuongezeka na kusababisha soko la kimataifa kutegemea mahitaji makubwa ya zao hilo.

Miaka ya nyuma hapa nchini mkonge ulikuwa ukilimwa katika mikoa miwili ukilinganisha na hali ya hewa ya eneo husika ambayo ni Morogoro na Tanga.

Kwa sasa zao hilo limeshika kasi na kuanza kulimwa katika Wilaya ya Kishapu, Shinyanga, kama zao la biashara tofauti na awali ambapo pamba ndiyo lilikuwa zao kuu la biashara.

Suzane3 Suzan Jinyange (53), ni mkulima wa katani na msindikaji wa zao hilo kutoka Kishapu mkoani Shinyanga, anasema zao hilo limewaongezea mafanikio makubwa wakulima wilayani humo.

Anasema yeye ni mama wa nyumbani, ameolewa na ana watoto sita, amejikita katika zao hilo tangu mwaka 2013.

“Awali nilikuwa nikilima mazao ya  kawaida lakini nilipoanza kufanya biashara hii ya mkonge kwa kulima na kusindika nimepata mafanikio makubwa,” anasema.

Anasema wakati anaanza alipanda robo tatu ya heka na kununua mkonge kwa wakulima heka mbili kwa ajili ya kusindika.

Anasema kwa mwaka anaweza kusindika tani 10 na kuuza kwa makampuni ya mkonge ambapo kilo moja huuzwa kati ya Sh 800 hadi 1,000 na kama mkonge aliosindika ni mzuri zaidi hufikia Sh 1,200 hadi 1,300.

“Nalishukuru Shirika la Oxfam kupitia miradi yao kwani limetupatia elimu juu ya zao hili kwa sababu ardhi yetu ni kame mno, tulikuwa tunapata hasara na kujikuta maendeleo ya kiuchumi yanarudi nyuma kila siku,” anasema.

Mkulima huyo anasema hivi sasa wanapopanda mikonge katikati huchanganya na mazao mengine kama vile mahindi, choroko na karanga.

Jinyange anasema Shirika hilo kupitia wataalamu wake wamebadilisha maisha yake kwa kumpatia mashine ya kusindika mkonge na kupatiwa elimu zaidi juu ya kilimo hicho.

“Nimefanikiwa kununua mashamba, kusomesha watoto pamoja na kumuuguza mtoto wangu anayesumbuliwa na saratani ya mguu.

“Nilikuwa sina meno yaling’oka ila nilipata fedha za kununua meno bandia, pia nimewaajiri vijana ambao wananisaidia shughuli zangu za kusindika mkonge,”anasema.

Kwa Upande wake Kaimu Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Wilaya ya Kishapu, Godwin Evarist, anasema Shirika la Oxfam liliingia katika wilaya yao mwaka 2009 na kuanza shughuli zake katika vijiji 10 na baadae kuongeza kasi ya vijiji 30 kwa kuelimisha jamii  juu ya matumizi ya zao la mkonge.

Anasema awali watu walikuwa wanatumia zao hilo kama mipaka ya kutenganisha shamba la mtu mmoja na mwingine lakini baada ya kupatiwa elimu wameweza kupiga hatua kutoka katika mipaka hadi kuwa zao la biashara.

Evarist anasema wametambua kuwa zao hilo ni la uchumi hivyo wameamua kuhamasisha wakulima kuacha dhana ya kupanda mipaka pekee bali walipande mashambani.

“Zao hili ni mkombozi katika kuwaletea kipato wakulima wa Kishapu, kwa sababu awali walikuwa wakitegemea zao la pamba ambapo lilikuwa lina changamoto nyingi. Hivyo kuanzishwa kwa zao hili wakulima wameona watajikomboa kwani wengi wamehamasika na wameanza kuchangamkia fursa,”anasema

Anasema kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17, wamelichukua zao hilo na kuliingiza katika mipango yao ya halmashauri  ambapo wametenga Sh milioni 200 kwa ajili ya kuliendeleza.

Ofisa huyo anasema kupitia fedha hizo wataviwezesha vikundi vya kina mama kwa kuwapatia mbegu pamoja na mitaji midogo midogo ya kuendeleza zao hilo.

Anasema kutokana na wakulima wengi kuhamasika kumekuwa na uhaba wa miche ya mkonge hivyo mpango wa halmashauri ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kitalu cha miche 25 ili kuwe na miche ya kutosha.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ng’umbi, anasema watahakikisha zao hilo linapewa kipaumbele na kuleta tija kwa wakulima wa wilaya hiyo.

Anasema tangu zao hilo lianze kulimwa limeweza kusaidia wakulima kuishi katika mazingira mazuri kwa kusomesha watoto wao na pia kupata kipato cha kutunza familia.

Ng’umbi anasema wamekuwa wakihamasisha katika mikutano ya hadhara pamoja na kulima mazao mengine na kwamba wakulima wanapaswa kulima mkonge kutokana na zao hilo kustahimili hali ya ukame.

“Tumeanza kuhamasisha katika shule, kaya na hata kata kupanda mikonge walau heka mbili, tunaishukuru Oxfam kwa kutoa elimu kwa wakulima wetu na wengi wamepata mafanikio kupitia zao hilo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles