26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkoa wa Dodoma kujenga mitaro miwili kukabiliana na mafuriko

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Kutokana na athari za mafuriko katika Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma, Mkoa huo umejipanga kuchimba na kujenga mitaro miwili mikubwa ambapo mmoja utatiririsha maji kutoka kwenye mabwawa hayo na mwingine utakaokinga maji ya mtiririko pembezoni mwa barabara kuu ya Dodoma kwenda Singida.

Hatua hiyo imekuja kufuatia wakazi wa mitaa ya Bochela, Salama, Mtube na Mnyakongo katika Kata ya Nkuhungu Jijini hapa kukumbwa na mafuriko hali ambayo imesababisha kukimbia nyumba zao na hivyo kuishi kwa majirani, ndugu jamaa na marafiki huku wengine wakiishi katika shule ya Msingi Mnyakongo.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Binilith Mahenge amefika leo Jumapili, Mei 9, 2021 katika eneo hilo akiwa na Kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa  Wilaya ya Dodoma Mjini, Josephat Maganga na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde.

Akiwa katika eneo la tukio pamoja na wakazi walioathirika na mafuriko hayo RC Mahenge amepokea taarifa ya kikosi kazi alichokiunda ya hali halisi ya mafuriko na mapendekezo ya kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma amesema wataalamu wameshauri maji yaliyopo katika eneo hilo yanatakiwa kupunguzwa kwa kujengwa mitaro miwili mikubwa ambapo mmoja utatiririsha maji yatakayozidi kutoka kwenye mabwawa hayo na mwingine utakaokinga maji ya mtiririko pembezoni mwa barabara kuu ya Dodoma kwenda Singida.

“Hamu yetu tungetaka sana kuwarejesha wananchi katika makazi yao lakini wataalamu wanashauri kwamba kitu cha kwanza lazima tuyazuie maji yanayoingia hapa kutahitajika kujenga mtaro kutoka pale Shell mtaro mkubwa.

“Pili wanapendekeza lazima tutengeneze mtaro kutoka kwenye bwawa kwa sababu hapa tupo chini kiwango cha mita tano kwahiyo ni kazi kubwa na ni ya gharama hatuna uhakika itazuia maji kiasi gani,”amesema.

Amesema Serikali imejipanga kupeleka mapendekezo hayo Serikalini ambapo kesho, Mkuu huyo wa Mkoa anatarajia kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kuzungumzia jambo hilo pamoja na kuomba fedha.

“Kwa hiyo tunasema hapa lazima tuandae namna ya kuwasaidia wananchi wetu tunasema kwanza serikali imejipanga na tutapeleka haya mapendekezo lakini ujenzi wake hauwezi kukamilika mpaka Desemba tunahitaji kuomba fedha,”amesema Dk. Mahenge.

Dk. Mahenge amesema wakati mipango hiyo ikiendelea Serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Jiji la Dodoma imetoa zaidi ya viwanja 500 katika maeneo ya Nala na Mahomanyika kwa ajili ya waathirika hao vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni mbili bure kwa wakazi hao.

Amesema pamoja na kuwapa viwanja mbadala hakuna mwananchi yeyote ambaye atanyang’anywa eneo lake lilozingirwa na maji.

“Wakati mipango hii inaendelea wananchi wetu sisi kama serikali tupo tayari kuwapa viwanja mbadala vya kuanza maisha  mengine. Lakini tunasema baada ya hii  mikakati kufanyika endapo maji yataziacha nyumba zitakuwa salama ambazo leo zipo katika maji yale maeneo ambayo wanayamiliki ni ya kwao na ndio maana nimekuja na orodha ya waathirika ili baade tukikubalina hii tunaitunza umiliki wako hauchukuliwi na mtu yeyote,”amesema.

Awali akiwasilisha taarifa ya kikosi kazi,Mwenyekiti wa kamati hiyo, Michael Maganga amesema wanapendekeza eneo lenye ukubwa wa ekari 147 litangazwe kama eneo hatarishi na kutokufaa kwa makazi ya binadamu.

Pia, wanapendekeza kufanyiwe maboresho ya mabwawa hayo kwa kuondoa tope ili kuongeza kina pamoja na kuimarisha kina na kujengea uzio ili kuzua watu hasa watoto  wasiingie ndani.

Vilevile, Halmashauri ya Jiji isitishe zoezi la urasimishaji katika mitaa ya Bochela na Mtube kwani ni hatarishi,pia izuie shughuli mbalimbali za kibinadamu pamoja na viwanja vilivyopimwa na kumilikishwa ambavyo havijaendelezwa isitishe utoaji wa vibali vya ujenzi.

Naye, Mbunge Mavunde alimwomba Mkuu wa Mkoa maji yaliyopo katika eneo hilo yatumike kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali Jijini hapa kauli ambayo iliungwa mkono na RC Mahenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles