25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

MKIMALIZA KUKAMATA CD BANDIA TAZAMENI HAYA

NA MWANDISHI WETU

WIKI hii kwenye tasnia ya burudani, habari iliyochukua uzito wa juu ni kitendo cha baadhi ya wasanii wa filamu kuandamana, wakipinga uuzwaji wa filamu za nje zisizofuata utaratibu walizodai zinaua soko lao.

Binafsi sijaona sababu ya msingi ya kuandamana wakati kuna mambo ambayo hayajakaa sawa ndani ya tasnia yenyewe. Hapa nakusogezea mambo makuu manne ambayo ndiyo chanzo cha soko la filamu kuporomoka.

Jambo la kwanza ni elimu, mipango na malengo. Utaona wasanii na waongozaji wakubwa na matajiri duniani wengi wao wana elimu kubwa ya sanaa hiyo, wamesoma, hivyo wana uelewa mkubwa na kile wanachokifanya kinachochangia mipango na malengo yao kufanikiwa, wasanii wa Bongo jitazameni kwa hili.

Jambo la pili ni maudhui. Huu ndio uhai wa filamu, hapa ndipo palipoporomosha soko la filamu, utaona licha ya Tanzania kuwa na watunzi mahiri wa riwaya na hadithi za kusisimua kama kina Eric Shigongo, Fredrick Bundala, Hussein Tuwa na wengine, lakini wasanii wetu hawawatumii hawa kwenye kazi zao na badala yake kila kitu wanafanya wao, dunia ya leo haitaki hivyo, ni lazima majukumu yagawanywe, watu wenye kazi zao wapige mzigo.

Jambo la tatu ni uzalishaji. Bongo Fleva ilianza kupotea lakini wakaibuka wasanii kama kina AY, Vanessa, Diamond, Ali Kiba na wengine wakavuka mipaka ya nchi kwenye kutafuta watayarishaji bora wa filamu na hapo ndipo muziki wao ukashika chati.

Sasa nyinyi mkishamaliza kuzuia filamu za nje, jaribuni kusafiri, nendeni hata Nigeria mkajaribu kutengeneza kazi zetu huko halafu muone kama mtaendelea kumtafuta mchawi anayeua soko leo.

Jambo la mwisho na muhimu ni kutafuta masoko. Inakuwaje msanii wa kisasa unategemea CD? Jifunzeni kitu kwa wasanii wa Bongo Fleva wanapouza muziki wao kidijitali. Soko kubwa la filamu lipo kwenye chaneli kama Netflix, huko ndiko biashara inafanyika.

Binafsi nilidhani badala ya kuandamana mngekutana na viongozi hao wa Serikali muombe kuwezeshwa ili mpate angalau Movie Theatre, ili muache kutegemea CD kwenye ulimwengu huu wa dijitali.

Zingatieni hayo mambo manne na kama hamuwezi kuingia shule kupata elimu ya sanaa, basi siyo dhambi kusafiri kwenda nje ya nchi kujifunza kwa wasanii wenzenu ili muyalete hayo maarifa nyumbani kwa ajili ya kuokoa soka la filamu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,227FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles