Aveline Kitomary , Dar es salaam
MAMLAKA ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inatarajia kuanzisha mfumo wa kanzidata wa Taifa katika upimaji wa sampuli za vinasaba (DNA), utakaosaidia kurahisisha utambuzi wa miili iliyoharibika na watu wanaojihusisha uhalifu kwa kurahisisha uchunguzi na kutokutumia ndugu.
Mfumo huo pia utatumiwa katika kurahisisha huduma za matibabu kwa kuangali mfanano wa vinasaba unaolingana kwa ndugu wa karibu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, wakati akitoa tathimini ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Mgufuli, Mkemia Mkuu wa Serikali Dk. Fidelice Mafumiko, alisema kuwa mfumo huo pia utatumika kwa watoto wa mtaani ambao wametelekezwa na wazazi wao.
“Tunataka tutumie kipindi cha miaka miwili kwamba hilo suala likamilike hilo linaenda hatua kwa hatua na inahitaji umakini mkubwa ambapo tuitashirikiana na taasisi zingine kama NIDA na RITA mfumo huo utasaidia utambuzi katika miili iliyoharibika.
“Lakini hii ni tofauti ukiwa na database badala ya kutafuta ndugu tunawapata kupitia mfumo huo pia itasaidia sana kwenye uhalifu mfano ubakaji ,mauaji ya kutumia silaha sasa tunapoanza kutumia mfumo wa database tutaweza kuwatambua.
“Pia itatumika katika matibabu tutashirikiana na madaktari katika kuwasaidia kugundua DNA ambazo zinafanana mfano mtu akitaka kumtolea ndugu yake figo mfumo utaonesha nani ana uhusiano na anastahili ampatie mgonjwa figo kati ya ndugu,” alisema.
Alisema faida nyingine ya mfumo huo pia utahusika katika suala zima la mirathi na uhalifu wa makosa ya jinai kama wizi, ubakaji, mauaji na majanga.
Alibainishha kuwa mfumo huo utaanza kwa watoto ambao wanazaliwa,katika mifumo ya matibabu na mahakamani.
Akielezea mafanikio waliyopata kwa miaka mine alisema tayari wameshafanya uwekezaji katika miundombinu ya maabara za uchunguzi ikiwamo vifaa na majengo.
“Tumenunua mitambo yenye thamani ya bill 6.5 hizi ni mashine za kisasa za upimaji wa DNA 9 mpya, pia matumizi ya Tehama yameimarika kama matumnizi ya mfumo wa elektroniki, mifumo ya usajili wa wadau wa kemikali kwa njia ya mtandao, mfumo wa usimamizi wa fedha kuna malipo ya serikali na hata majengo tumejipanua tuko ukanda wa mikoa sita nchini,” alisema
Aidha alisema kuwa kwa kipindi cha miaka minne mapato ya mamlaka yameongezeka kutoka Sh bilioni 9.342 mwaka 2015 na 2016 na kufikia Sh bilioni 24.246 kwa mwaka 2018 hadi 2019.