30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

MKEMIA: DNA HAICHUNGUZI MTOTO ALIYE TUMBONI

NA PENDO FUNDISHA-MBEYA


OFISI ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema mtambo wa kufanya uchunguzi wa kimaabara, hautahusika na uchunguzi wa vinasaba vya mtoto aliye tumboni kwa mama yake (DNA).

Kauli hiyo imetolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samweli Manyele, wakati akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wadau waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa mtambo mpya na wa kisasa wa aina ya Energy Dispensive X-Ray Fluorescence(ED-XRF) kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kimaabara.

Awali akiuliza swali hilo, Joseph Martin kutoka idara ya afya, alitaka kufahamishwa kama mtambo huo utasaidia kubaini baba wa mtoto kabla ajazaliwa, lengo likiwa ni kuharakisha  utoaji wa maamuzi wa kesi mahakamani.

Alisema maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni taasisi muhimu yenye majukumu ya kufanya uchunguzi wa kimaabara pamoja na usimamizi wa sheria zilizo chini ya wakala, hivyo kisheria na taratibu za kazi haziwaruhusu wao kupima DNA kwa mtoto aliye tumboni.

“Taratibu na sheria za kazi hii wataalamu hawaruhusiwi kupima mtoto aliye tumboni, ni mpaka azaliwe kisha zoezi hilo kufanyika lengo kuu ni kulinda haki za mtoto, lakini kubwa zaidi ni kwamba maabara hii inashughulika na upimaji wa sampuli chini ya usimamizi wa sheria ya wakala,” alisema.

Mkemia Mkuu alizitaja baadhi ya kazi zitakazofanywa na maabara hiyo ni pamoja na kuhakiki ubora na usalama wa bidhaa, sampuli za mazingira, sampuli zinazohusisha makosa ya jinai kama vile sampuli za vinasaba na dawa za kulevya.

“Awali vipimo vya namna hii vilikuwa vikifanyika jijini Dar es Salaam tu, ofisi za mikoa zilikuwa zikifanya kazi ya kukusanya sampuli na kusafirisha, lakini sasa mtambo umesimikwa Mbeya na utatumiwa na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kufanya kazi hiyo,” alisema. 

 “Maabara inachangia katika kutekeleza sera ya afya ya mwaka 2007 kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara  kwa kuhakiki ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa viwandani,” alisema Profesa Manyele.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, alitoa wito kwa viwanda, mashirika, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kutumia huduma zinazotolewa na maabara ya mkemia mkuu wa serikali ili kuhakiki ubora wa  bidhaa zinazozalishwa  viwandani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles