MKE WA SCHWEINSTEIGER ASTAAFU TENISI

0
769

BELGRADE, SERBIA


ana-ivanovicBINGWA wa zamani namba moja wa mchezo wa tenisi duniani kwa upande wa wanawake, Ana Ivanovic, ambaye ni mke wa nyota wa soka wa klabu ya Man United, Bastian Schweinsteiger, ametangaza kustaafu mchezo huo baada ya kumaliza msimu huu huku akiwa majeruhi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, aliwahi kushika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani mwaka 2008 baada ya kufanya vizuri katika michuano ya French Open.

Mwaka huu tangu umeanza mchezaji huyo amefanikiwa kucheza jumla ya michezo 15 kabla ya kuwa benchi tangu Agosti mwaka huu alipoumia kwenye michuano ya US Open.

Kupitia akaunti yake ya Facebook, mchezaji huyo juzi alitangaza kustaafu mchezo huo. “Ninaamini ninafanya maamuzi magumu lakini kuna wakati natakiwa kuyafurahia maamuzi haya, wala si jambo baya ila ni maamuzi ambayo yalitakiwa niyafanye.

“Kulikuwa na mambo mengi ambayo yanaendelea juu yangu katika maisha ya mchezo huu wa tenisi, wapo ambao walitaka nisiendelee na mchezo huu, lakini haukuwa muda sahihi, ila sasa ni muda sahihi.

“Katika maisha yangu ya mchezo huu nimepitia nyakati tofauti, kuna wakati nilitamani kuachana kabisa na mchezo huu, lakini nilipambana huku nikiwa na lengo la kufika mbali, nashukuru nimefanikiwa kutimiza malengo yangu.

“Lakini kwa msimu wa mwaka huu, nilikuwa katika kipindi kigumu katika mchezo huu kutokana na kuwa majeruhi, najua kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa wananiangalia mimi hasa vijana wadogo wa kiume na kike, lakini kutokana na kukaa nje kwa muda mrefu nimeona bora nifanye maamuzi haya,” alisema Ana.

Nyota huyo alifanikiwa kufunga ndoa wakati wa majira ya joto mwaka huu na kiungo wa Man United ambaye kwa sasa hana nafasi kubwa ndani ya kikosi hicho, Bastian Schweinsteiger.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here