KIAMBU, KENYA
MKE wa Naibu Rais William Ruto, Rachel Ruto juzi aliongoza maombi maalumu kwa wanawake waliokiri kuwa tasa katika Kaunti ya Kiambu.
Makumi ya wanawake hao walimwendea Ruto wakimtaka awaombee.
Bila kusita, Ruto aliwaelekeza kwa magoti huku wakiwa wameshikana mikono na kuanza maombi yaliyodumu dakika 25 akiwaombea kwa Mwenyezi Mungu.
“Waone hawa waja wako Mwenyezi Mungu. Wanalia kuwa wangetaka kumshika mtoto. Baba Mungu teremsha baraka zako za rehema na uwape hakikisho kuwa imani yao imewaponya utasa wao,” aliomba Ruto.
Ruto aliendesha mlolongo wa mikutano ya maombi katika kaunti mbalimbali za hapa akilenga amani katika msimu huu wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, 2017.
Awali, alikuwa ameongoza hafla ya maombi katika uwanja wa Ihura ulioko kaunti ya Murang’a kabla ya kuelekea hapa.