MKE WA MZEE MAJUTO AOMBA MSAADA

0
752

JEREMIA ERNEST NA KELVIN SHANGALI (TUDACO)             |                


ZIKIWA zimepita siku 13 toka afariki mchekeshaji nyota nchini, Amir Athuman ‘Mzee Majuto’, mke wake wa mwisho, Aisha Mbwana Yusuph, amelazimika kuja jijini Dar es Salaam kuomba msaada, baada ya kuambiwa na ndugu wa marehemu kuwa hatasaidiwa kwa chochote.

Aisha ambaye aliolewa na Mzeee Majuto mwaka 1997 na kubahatika kupata watoto wanne ambao ni Bilali (17), Halima (12), Rutifia (5) na Yusra (3), amesema alikuwa anaishi Tanga maeneo ya Donge katika kipindi chote cha maisha yake na Mzee Majuto.

Akizungumza na MTANZANIA, mke huyo wa Mzee Majuto ambaye kwa sasa anaishi Vingunguti Machinjioni, Dar es Salaam, alisema tangu msiba huo uishe, hakuna mtu yeyote aliyemjali kwa kula na mahitaji mengine kutoka kwa ndugu wa mchekeshaji huyo.

“Tulikaa kikao cha familia, walikubali kunipatia huduma zote za eda ila tulipomaliza siku mbili nilipokea ujumbe kutoka kwa mjomba wa marehemu, akisema hawataweza kunipatia huduma ya aina yoyote, nitafute mbinu ya kujisaidia na watoto wangu,” alisema Aisha.

Aisha alikiri hakuna aliyemfukuza kwenye nyumba, ila kauli ya kutopata huduma ni sawa na kuambiwa atoke akatafute jinsi ya kumudu maisha yake.

MTANZANIA lilimtafuta Hamza Kasongo ambaye ni mjomba wa Mzee Majuto, alisema hajatoa kauli yoyote au  kuongea na mke wa marehemu, huku akisisitiza kuwa kila kitu kitajulikana siku ya 40 ambayo ni Septemba 14, mwaka huu.

“Sisi hatujaongea chochote na mke wa marehemu, mara ya mwisho niliwasiliana naye hata kabla ya mume wake hajafariki, siwezi kusema chochote, hadi siku ya arobaini ambayo itakuwa Septemba 14 hadi 15,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here