Mke asema mumewe hayuko sawa baada ya kutekwa

0
863

Bethsheba Wambura-DAR ES SALAAM

MKE wa mfanyabiashara Raphael Ongangi raia wa Kenya, aliyedaiwa kutekwa wiki iliyopita, Veronica Kundya amesema licha ya mumewe kupatikana akiwa salama na mwenye afya njema lakini kiakili bado hayuko sawa.

Katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Veronica amesema mumewe anaonekana kama mtu mwenye wasiwasi na hofu ya kutekwa tena baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana kwa siku nane.

Ongangi alipatikana Jumanne Julai 2, mwaka huu Mombasa nchini Kenya karibu na nyumbani kwa shangazi yake baada ya kutekwa na watu wasiojulikana maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam Juni 24, mwaka huu.

“Kiafya yuko vizuri, hajaumia, hajafanya chochote. Lakini nadhani katika hizo siku nane alizopitia kama zilivyokuwa ngumu kwangu ila naamini zilikuwa ngumu zaidi kwake yeye, kiakili bado hayuko sawa kwasababu alikuwa na hao watu hajui chochote, hajui kesho yake itakuwaje.

“Nilipokutana naye usiku hapa Mombasa nilimkumbatia kwa nguvu sana na sikuamini kama ni yeye namuona ni kama ile siku tuliyofunga ndoa ile furaha niliyokuwa nayo, kilichokuwa kinanipa nguvu niliamini anatafutwa na ilikuwa ngumu sana kwa kweli.

“Kiakili bado ana wasiwasi wa  usalama wake, lakini naamini kama yuko hapa na sisi sasa hivi na Mungu kama Mungu amesababisha awe hapa basi naamini atakuwa sawa tu,” amesema Veronica.

Aidha, Veronica amerudia kutoa shukrani kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao walijitolea na kutuma ujumbe wa kutaka mumewe Ongangi arudishwe.

“Ningependa kumshukuru Mungu sana kwa sababu yeye amesikia maombi yetu, nilikuwa nasema Mungu asingeacha kusikia maombi ya Afrika Mashriki yote, na hii ilinipa nguvu kuwa atarudi, nisingependa mtu mwingine ajisikie nilivyojisikia,” alisema Veronica kwa simanzi iliyochanganyika na furaha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here