24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa: Raila alinitoa jasho

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

KATIKA kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’  (Maisha yangu, Kusudio langu), Rais mstaafu Benjamin Mkapa amefichua mengi, lakini zaidi anasema hatasahau mgogoro wa Kenya baada ya Uchaguzu Mkuu wa nchi hiyo Desemba mwaka juzi ulivyompa changamoto mpya maishani.

Katika kumbukizi yake, Mkapa anasema baada ya kuondoka madarakani Novemba 2005, alikuwa katika mapumziko akiwa hajapata majukumu makubwa tena, hadi zilipoibuka vurugu za baada ya uchaguzi huo wa Kenya.

Anasema vurugu hizo ndizo zilizompa jukumu jipya la kuwa msuluhishi, katika mazingira ambayo hata hakuyatarajia, lakini anakumbuka zaidi namna pande zote zilivyokuwa ngumu kukubali usuluhishi huo.

Mkapa anasema baada ya kuibuka kwa mgogoro huo ambao upinzani ulikataa kukubali matokeo na watu kuanza vurugu, aliyekuwa Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano chini ya mwamvuli wa Wakuu wa Nchi Wastaafu wa Afrika, alimpigia simu yeye, Rais wa zamani wa Botswana, Ketumile Massire na Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda kuwataka wawahi kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Anasema walifika Nairobi na mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa ni kiongozi wa upinzani kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, ambaye alikuwa akidai kuporwa ushindi na aliyekuwa Rais wa Kenya, Mwai Kibaki.

“Majadiliano ya usuluhishi yalianza, japokuwa pande zote walikuwa wagumu sana katika hili. Tulikutana na kila upande kwa wakati tofauti, kisha tukawakutanisha. Walikuwa wabishi sana na ilifikia hatua niliona kama wanaelekea kukabana makoo.

“Suala zito katika mabishano hapa lilikuwa ni nani aliyeshinda uchaguzi hadi tulipoingilia na kusema mambo yameshaharibika na kuendelea mabishano ni kuendeleza fujo na mauaji. Hivyo suala muhimu ilikuwa kuangalia namna ambavyo nchi ingeendeshwa kwa maridhiano ya pande zote,” anasema Mkapa.

Anasema hilo halikuwa suala jepesi kwa pande zote, hasa kwa Raila ambaye aliamini ndiye mshindi aliyeporwa ushindi wake na kwa kuwa kila upande ulitaka upewe madaraka kamili.

“Ilikuwa ngumu sana kuwafanya ODM wamkubali Kibaki kama Rais, ila alipokwenda Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa Mwenyekiti mpya wa AU, alitoa pendekezo kuwa timu ya usuluhishi ikutane na Kibaki na Odinga kwa pamoja,” anasema Mkapa.

Anasema hilo liliwezekana na wakiongozana na wanasheria wao, walijifungia ndani hadi walipofikia makubaliano, baada ya kusisitiza kwa wawili hao kuwa suala la msingi ni kuheshimiana na kuelewana na hatimaye, waliona umuhimu wa kumaliza suala hilo kwa kuwa tayari matokeo yalishaleta athari kwa nchi hiyo.

Mkapa anasema waligundua pia uwepo wa aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kibaki, Martha Karua na William Ruto aliyekuwa mtata akimwakilisha Odinga kulikuwa kukiwakwamisha.

Kutokana na hali hiyo, anasema walitumia mbinu ya kuwaweka kando na kukutana na Kibaki na Odinga pekee na kilichofuata ilikuwa ni kushuhudia makubaliano ya Serikali ya pamoja yakitiwa saini.

“Ninajivunia nafasi yangu ya kuwa msuluhishi katika mgogoro huo uliokuwa mgumu wa Kenya. Hapo nilipata pia nafasi ya kufanya kazi na aliyekuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan ambaye alikuwa msikivu, akiuliza maswali mengi, lakini akizungumza kwa ustadi mkubwa na pande zote mbili,” anasema.

KUUZA NYUMBA ZA SERIKALI

Mkapa anasema uamuzi wa kuuza nyumba za Serikali haukuwa mwepesi, lakini aliamua hivyo kwa kuwa gharama ya kuzitunza ilikuwa kubwa na kwa wakati huo, zilikuwepo nyumba 6,000 tu, hivyo ni asilimia tatu tu ya wafanyakazi wa umma waliokuwa kwenye nyumba hizo.

Anasema pia kuna baadhi ya watumishi ambao walikuwa na tabia ya kutoheshimu mali za Serikali na nyumba nyingi zilikuwa hazifanyiwi hata usafi, nyingine zilitumiwa kufugia kuku na ng’ombe, kwa hiyo waliangalia suala hilo kwa mapana kabla ya kuchukua uamuzi wa kuziuza.

“Katika hili, tuliangalia watu wa muhimu ambao kwa majukumu na mamlaka yao wanaweza kubaki na nyumba za Serikali, katika mikoa tuliangalia wale ambao Rais akienda huko anaweza kufikia kwao, hiyo ikaweka msingi wa maamuzi yetu, kwamba hao ndio watakaobaki na nyumba za Serikali, lakini wengine wote watalazimika kujitegemea kwa makazi,” anasema Mkapa.

Anasema yeye si wa kwanza kufanya hivyo kwa kuwa hata Mwalimu Nyerere alianzisha Shirika la Nyumba la Taifa (siyo hili la sasa) ambalo kazi yake kubwa ilikuwa kujenga nyumba na kuziuza kwa watumishi wa umma, suala ambalo lilifanyika pia huko Msumbiji, Lesotho na Zambia kwa wakati huo.

Mkapa anasema alibaini kuwa kuna upungufu katika suala la soko la nyumba, kwa hiyo mwaka 2002 aliamua kuunda Wakala wa Majengo (TBA) ambao ulipewa jukumu la kujenga nyumba za kupangisha na za kuwauzia watumishi wa umma, ambao wangekopeshwa kwa riba na wengine wangepewa umiliki kila baada ya miaka 25.

 “Katika hili sikufanya upandeleo, niliwapa wale waliokaa kwenye makazi hayo nafasi ya kununua nyumba hizo kwa kuwa niliona wale waliopewa jukumu la kusimamia wanaweza kuwapuuza wale wenye kipato cha chini, ambao wasingeweza kununua makazi hayo kwa gharama zilizowekwa kibiashara,” anasema Mkapa.

Anasema baada ya kuchukua uamuzi huo, anakumbuka siku moja alipata barua kutoka kwa ofisa mmoja wa elimu wa kanda, aliyekuwa amekaribia kustaafu, akimwambia; “Ninashukuru sana mkuu, angalau na mimi sasa nina kitu cha kuonyesha kama sehemu ya utumishi wangu, nyumba yangu mwenyewe.”

Anasema kelele kuhusu uamuzi huo zilikuwa nyingi, lakini wakati wote amekuwa akiamini kuwa alifanya uamuzi sahihi, kwa kuwa uliokoa gharama kubwa ya kukarabati na kuzitunza nyumba hizo, ni fedha nyingi sana kwa nchi masikini kama Tanzania.

KUNUNUA NDEGE YA RAIS

Mkapa anasema suala jingine lililoibua mjadala mpana wakati wa utawala wake ndani na nje, lilikuwa ni la kununua ndege ya rais.

Anasema wakati huo, ndege ya Serikali ilikuwa ni ya aina ya Fokker jet, lakini ilikuwa haina kasi ya kutosha na ilikuwa ni gharama sana kuifanyia matengenezo.

Mkapa anasema ndege hiyo ilikuwa na miaka 24 tangu iliponunuliwa na tayari uzalishaji wa ndege za aina hiyo ulishasitishwa tangu mwaka 1987, na kutokana na ukubwa wake, ilihitaji kusafiri na watu wengi, suala ambalo halikuwa kipaumbele chake.

“Kwa hiyo, niliamua kuwa iwapo tutakuwa na ndege ndogo yenye kasi na inayoweza kusafiri umbali mrefu zaidi, itamwezesha Rais kusafiri kwa haraka katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) suala ambalo lina tija kwa diplomasia ya ujirani na muhimu pale inapotokea shida.

“Utasafiri kwa uhuru zaidi, unaweza kuweka kituo hapa na pale kwa ajili ya mazungumzo na watu muhimu, pia ndege ndogo inapunguza hata idadi ya watu unaosafiri nao, unaweza kusafiri na watu 12 tu, hatua ambayo ingesaidia hata kupunguza malalamiko ya wale ambao watabaki na kupunguza hata gharama za posho,” anasema Mkapa.

Anasema kulikuwa na mijadala kadhaa iliyokuwa ikiendelea katika baraza lake la mawaziri, Bunge na wafadhili, wengi wakipinga ununuzi wa ndege hiyo, hasa baada ya kuwa nchi imepata msamaha wa madeni.

Benki ya Dunia, IMF na baadhi ya washirika wa maendeleo walitaka kupata maelezo ya kina kwanini Rais anataka ndege mpya, japokuwa walikuwa wakijua udhaifu wa ndege ya Fokker jet.

“Waziri wangu wa Fedha wakati huo, Basil Mramba alisimama kidete kwa ajili ya ununuzi wa ndege hiyo, niliambiwa kwamba alisisitiza kuwa ‘ndege itanunuliwa hata kama watu watakula nyasi’, alisisitiza kuwa hata kama tumepewa msamaha wa mikopo, hiyo si sababu ya kumfanya Rais wetu atumie punda kusafiri,” anasema Mkapa.

Anasema hadhani kama kungekuwa na ukinzani iwapo uamuzi huo ungechukuliwa na nchi iliyoendelea, lakini wafadhili walikuwa wakijaribu kujenga picha kwamba tunatumia fedha za Serikali kununua ndege, japokuwa hali ya kiuchumi katika ngwe yake ya pili haikuwa mbaya sana, kwa kuwa fedha zilikuwepo tofauti na pale tu alipoingia madarakani.

Mkapa anasema pamoja na ukinzani na kukosolewa kwa uamuzi huo, alichagua kuusimamia akiamini kuwa atakapokuwa amemaliza muhula wake wa urais, angalau vyombo vya habari vitang’amua kuwa hakuchukua uamuzi huo ili kutimiza matakwa yake binafsi.

Anasema alijua pia kuwa Rais atakayefuata baada yake, huenda pia angeweza kuogopa kununua ndege ya aina hiyo, kwa hiyo alimwambia kuwa anamwachia ofisi akijua kuwa kama ni mawe yatarushwa kwake, lakini anamwachia ndege ikiwa tayari imeshanunuliwa.

Mkapa anasema pamoja na mageuzi aliyoyataja, walifikia hatua kwamba kila mmoja alikubali kuwa ni jambo lisiloepukika, kuwa lazima mageuzi yafanyike ili kufikia malengo waliyokuwa wamejiwekea, ya kuwa na uchumi unaokua kwa uhakika.

“Ukweli ni kwamba asilimia 10 ya ziada ya kura nilizopata wakati nikiwania muhula wa pili, ilikuwa ni ushahidi wa kazi nzuri niliyokuwa nikifanya, hii ilimaanisha kuwa wananchi waliniambia songa mbele, endelea,” anasema Mkapa.

VITABU VYAADIMIKA SOKONI      

Hadi kufikia jana, siku mbili baada ya kuzinduliwa kwa kitabu hicho Novemba 12, taarifa zilieleza kuwa tayari kilimalizika katika baadhi ya maduka ya kuuzia vitabu.

Katika tangazo lake, Duka la Vitabu la Tanzania Publishing House (TPH) lilieleza kuwa kitabu hicho kimemalizika na kwamba nakala zaidi ziko njiani, ambazo sasa zitauzwa kwa Sh 45,000 badala ya Sh 60,000 za awali.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota, Mkuki Bgoya alisema ni kweli kwamba nakala hizo za awali zimekwisha kwa kuwa zilikuwa chache, ambazo zilisafirishwa kwa ndege kuwahi uzinduzi ambao ulikuwa lazima ufanyike siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mkapa.

“Ni kweli, nakala zikizokuja mwanzo zilikuwa ni chache, kwa hiyo baada ya mauzo ya pale ukumbini, zilizobaki ndizo zilizopelekwa kwenye maduka ya vitabu. Ila nakala zaidi ziko njiani zinakuja kwa meli na zitakuwa tayari baada ya kama wiki tatu zijazo. Katika hizi, bei elekezi itakuwa ni Sh 45,000,” alisema Bgoya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles