25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Mkapa, Kikwete wajumuika na kina Kinana mazishi ya Iddi Simba

Leonard Mang’oha – Dar es Salaam

MARAIS wastaafu Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa wamewaongoza mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika mazishi ya Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara Iddi Simba.

Simba aliyefariki dunia Dar es Salaam juzi wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), alikuwa waziri kwenye Serikali ya Mkapa.

Mbali na marais hao wastaafu pia mazishi ya mwanasiasa huyo yalihudhuriwa na Makamu wa Rais Mstaafu, Ghalib Bilali, makatibu wakuu wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Wilson Mkama, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Dk. Edmund Mndolwa, Ispekta Jenerali wa Polisi mstaafu Said Mwema na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali.

Swala ya marehemu ilifanyika katika Msikiti wa Manyema Mtaa wa Lumumba kisha mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Mwinyi Mkuu Magomeni Mapipa, Kinodoni jijini hapa.

Akitoa salamu za chama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Dk. Edmund Mndolwa, alimwelezea Simba kama mtu aliyekuwa mnyenyekevu na mwenye upendo ka watu wote.

“Alikuwa mwenyekiti aliyenitanguliwa katika nafasi hii, niseme alikuwa mwenyekiti mwema na sisi kama chama tumesikitishwa zana na kifo hiki,” alisema Dk. Mndolwa.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali, alisema marehemu alitumia vema nafasi yake na kwamba alimaliza kwa heshima.

Wakati wa uhai wake Idd Simba aliwahi kuwa Mbunge wa Ilala (CCM), mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na kisha Waziri wa Viwanda na Biashara kwa miaka miwili – 2001 hadi 2002, kisha kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Katika nafasi yake ya uwaziri, Iddi Simba alilazimika kujiuzulu mwaka 2002, kutokana na kashfa ya uingizwaji wa sukari mbovu nchini.

Akiwa mbunge Iddi Simba, atakumbukwa kwa msimamo wake kutetea wazawa katika masuala mbalimbali, ikiwamo uwekezaji nchini.

Alilazimika kuandika kitabu kinachotetea uzawa jambo lililomfanya kutofautiana na sera za chama chake cha CCM.

Katika kitabu hicho aliwatetea Watanzania wazawa kwa kueleza kwamba wanastahili kuwekewa mazingira fulani ya kisera ili wajiendeleze na waendeleze rasilimali zilizopo.

Dhana hiyo ilipingwa na kuitwa ni dhana yenye kuchochea hisia za kibaguzi ambapo baadhi ya viongozi wa CCM wakati huo waliwatahadharisha wanachama wao kwamba dhana ya uzawa ni ya Iddi Simba na ni mawazo yake binafsi hayafungamani kabisa na sera za CCM.

Akiwa mbunge, Idd Simba aliwahi kukaririwa bungeni akisema kwamba lugha ya Kiingereza imesababisha Tanzania iwe na sheria mbaya zikiwamo za madini.

Alisema kuwa anaona aibu kwa kuwa alishiriki kupitisha sheria mbaya za madini zinazotumika kuinyonya nchi.

 “Zile sheria ni mbaya na mimi naona aibu kwamba zilipitishwa wakati nikiwa kwenye lile Bunge, lakini unatarajia nini wakati sheria zile zinatungwa kwa Kiingereza, na si wabunge wengi wanaoelewa lugha hiyo,” alisema Iddi Simba wakati huo.

Juni 19, 2013 Iddi Simba alifutiwa kesi iliyokuwa ikimkabili, iliyokuwa na mashtaka manne likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uda.

Kesi hiyo ilifutwa baada ya Wakili wa Serikali, Awamu Mbangwa kuwasilisha hati ya nuio la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kuifuta.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles